Amiri Jeshi Mkuu Sisi kuwania urais Misri
6 Februari 2014"Ndio,suala hilo limepatiwa maamuzi na sina chaguo bali kuitikia wito wa wananchi wa Misri.", hilo ndio lilikuwa jibu la Sisi wakati alipoulizwa na gazeti la Kuwait la Al-Seyassah iwapo alikuwa ameamuwa kugombania urais.
Katika mahojiano hayo yaliyochapishwa Ahamisi (05.02.2014) Sisi amesema "Wito wa wananchi umekuwa ukisikika kila mahala na sitoukataa. Nitaomba imani mpya ya wananchi kwa kupitia uchaguzi huru." Sisi aliwahi kufanya mahojiano na gazeti hilo huko nyuma ambapo alielezea nia yake ya kuwa rais.
Repoti hii inakuja wiki moja moja baada ya baraza kuu la kijeshi nchini Misri kumuidhinisha Amiri Jeshi Mkuu Sisi kuwa mgombea katika uchaguzi wa rais ambapo anahakikishiwa ushindi baada ya kumpinduwa rais aliechaguliwa kwa njia ya demokrasia Mohamed Mursi hapo mwezi wa Julai.
Umashuhuri mkubwa
Sisi amepata umashuhuri mkubwa kwa kumpinduwa Mursi mwenye msimamo wa itikadi kali za Kiislamu na sasa anatazamiwa kujiuzulu kama mkuu wa majeshi kabla ya kuwa mgombea rasmi katika uchaguzi wa rais uliopangwa kufanyika katikati ya mwezi wa Aprili.
Ushindi kwa Sisi mwenye umri wa miaka 59 ambaye atabidi avuwe mwagwanda yake ya kijeshi kwa ajili kushiriki katika uchaguzi huo utaendeleza desturi ya marais wa Misri kutokea jeshini tokea kupinduliwa kwa ufalme hapo mwaka 1952.
Sisi ameliambia gazeti hilo kwamba atahitaji msaada wa wananchi kutibu matatizo sugu ya Misri ambayo yamezidi kuwa makubwa katika miaka ya hivi karibuni.
Ahadi zake kwa wananchi
Sisi ambaye ni waziri wa ulinzi na mkuu wa baraza la kijeshi lenye nguvu kubwa nchini Misri ameonya kwamba hakuna dawa mjarabu ya kutibu mara moja matatizo ya Misri na hatojaribu kuwalaghai Wamisri.
Amesema hawatochezea ndoto zao au kuwaambia kwamba wana fimbo ya uchawi kutatuwa matatizo makubwa ya nchi hiyo.
Hata hivyo amesema hali ya usalama nchini Misri inaboreka na kwamba leo hali ni nzuri kuliko ilivyokuwa jana na kwamba kesho itakuwa nzuri zaidi.
Amesema iwapo atachaguliwa atatowa wito wa kuundwa kwa muungano wa nchi za Kiarabu kupambana na ugaidi unaozidi kukua katika eneo hilo.
Kutokomeza ugaidi
Sisi amesema watatowa wito wa kuwepo kwa Umoja wa Waarabu chini ya misingi ya ushirikiano katika ya nchi zenye kuathirika na ugaidi ili waweze kuendesha vita vya pamoja dhidi ya ugaidi.
Sisi anaamini kwamba nchi za Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) pamoja na nchi nyengine zitakuwemo katika umoja huo wenye lengo la kutokomeza tishio hilo la ugaidi.
Nchi wanachama wa GCC zikiwemo Saudi Arabia,Kuwait na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa wafadhili wakuu wa Misri tokea kupinduliwa kwa Mursi.
Hata hivyo kwa mujibu wa habari za karibuni jeshi la Misri limesema gazeti hilo la Kuwait limeitafsiri vibaya kauli hiyo ya Amiri Jeshi Mkuu Sisi kwamba atagombania urais na limesema kwamba atatangaza tu uamuzi wa aina hiyo kwa wananchi wa Misri.
Kwa wafuasi wake Sisi ni chaguo zuri kukomesha ukosefu wa utulivu wa miaka mitatu kufuatia vuguvugu la mwaka 2011 lililomuondowa madarakani Hosni Mubarak afisa mwengine wa kijeshi.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef