1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMISOM yaikomboa bandari ya Barawe

6 Oktoba 2014

Wanajeshi wa Somalia wakisaidiwa na wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika hapo jana wameikomboa bandari ya mwisho muhimu nchini Somalia iliyoshikiliwa na kundi la al-Shabaab.

Somalia Barawe Afrikanische Union AMISOM Soldaten Anti Al Shabab 05.10.2014
Picha: picture-alliance/AMISOM

Hatua ya kuukomboa mji wa bandari wa Barawe kutoka mikononi mwa kundi la al-Shabaab ni pigo jingine kubwa kwa kundi hilo ambalo lina mafungamano na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda na linakuja mwezi mmoja tu baada ya kifo cha kiongozi wake Ahmed Abdi Godane aliyeuawa katika shambulizi la kutokea angani lililofanywa na ndege ya Marekani isiyoruka na rubani.

Jeshi la kulinda amani la Umoja wa Afrika nchini Somalia – AMISOM, ambalo linawajumuisha wanajeshi 22,000 kutoka mataifa sita, limesema mji wa Barawe, ambao uko kilomita 200 kusini mashariki mwa mji mkuu Mogadishu, ulikombolewa bila “upinzani wowote kutoka kwa kundi hilo la kigaidi”.

Taarifa ya AMISOM imesema magaidi hao waliitumia bandari hiyo katika kuagiza silaha pamoja na kupokea wapiganaji wa kigeni. Aidha kundi hilo lilitumia Barawe kuuza mkaa katika mataifa ya Mashariki ya Kati, biashara iliyowaletea faida kubwa ya mamilioni ya dola yaliyotumiwa kama chanzo chao kikubwa cha ufadhili.

Wanajeshi wa kulinda amani wakishika doria katika mji wa Bulameer katika jimbo la Shabelle ya Chini, SomaliaPicha: Reuters/Tobin Jones

Gavana wa mkoa huo Abdukadir Mohamed Nur amesema hali sasa ni “tulivu na kuwa wapiganaji hao walitoroka kabla ya majeshi ya AMISOM kuufikia mji huo”. Watalaamu wanasema kuwa jambo la muhimu ni kuwa kile “mji mkuu” wa al-Shabaab umeanguka, na sasa wanamgambo hao ambao pia waliupoteza mji mwingine muhimu wa bandari ya Kismayo mnamo Oktoba 2012, sasa hawana miji mingine muhimu mikononi mwao.

Hussein Nur mhadhiri wa chuko kikuu kuhusu utawala mjini Mogadishu, anasema kando na kuwa kitega uchumi cha al-Shabaab, Barawe pia ilitumiwa kama ngome ya mafunzo kwa kundi hilo.

Hata hivyo, amesema kuwa kuanguka mji wa Barawe hakumaanishi kumalizika kwa vita dhidi ya kundi hilo, kwa sababu bado wanayadhibiti maeneo mengine makubwa ya mashinani. Al-Shabaab iliapa kulipiza kifo cha kiongozi wake na kuendelea kupigana ili kuiangusha serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa.

Siku ya Jumamosi, kamanda wa al-Shabaab Mohamed Abu Abdallah alisema kundi hilo litaendelea kuiwekea mbinyo jeshi la Somalia na la AU hataka kama wataupoteza mji wa Barawe. Lakini Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud aliuambia mkutano wa kilele wa Hadhara Kuu ya Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa al-Shabaab imefurushwa kutoka karibu asilimia 70 ya maeneo ya kusini na kati mwa Somalia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW