1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yazishutumu RSF, jeshi la Sudan kutenda uhalifu

3 Agosti 2023

Shirika la kimataifa la haki za binadamu Amnesty International katika ripoti yake mpya limezituhumu pande zinazozozana nchini Sudan kwa kutenda uhalifu wa kivita.

Logo der Organisation Amnesty International
Picha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Kulingana na ripoti hiyo iliyochapishwa leo Alhamisi, shirika la Amnesty International limesema mapigano kati ya majenerali wanaopingana nchini Sudan, ambayo yamekuwa yakiendelea kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, yamesababisha raia kushambuliwa kiholela na pia yamesababisha vifo vya raia wasiokuwa na hatia ikiwa ni pamoja na unyanyasaji wa kijinsia.

Wakimbizi wa Sudan kutoka jimbo la Darfur.Picha: ZOHRA BENSEMRA/REUTERS

Ripoti hiyo ya Amnesty International yenye kurasa 56 imesema raia waliuawa na wengine walijeruhiwa katika mashambulizi yaliyowalenga kimakusudi pia imetaja juu ya wanawake kubakwa, huku baadhi yao wakishikiliwa katika mazingira yanayolingana na utumwa wa ngono hasa katika mji mkuu, Khartoum, na eneo la magharibi ya nchi hiyo la Darfur.

Donatella Rovera, mwandishi mwenza wa ripoti hiyo, ameliambia shirika la habari la Associated Press kwamba unyanyasaji wa kijinsia umekuwa kipengele muhimu cha mzozo wa Sudan tangu mwanzo, na kwamba raia hawana nafasi ya kujichagulia wanachotaka, ni vigumu kwao kuondoka na wakati huo huo ni hatari sana kwao kukaa nchini mwao.

Kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan.Picha: El Tayeb Siddig/REUTERS

Kikosi cha Msaada wa Haraka, RSF na washirika wake wa makundi ya wanamgambo wa Kiarabu wamelaumiwa kwa takriban matukio yote ya ubakaji. Ripoti hiyo imesema wanachama wa RSF, waliwateka kinamama 24 na wasichana wapatao 12 na kuwashikilia kwa siku kadhaa ambapo walibakwa na wanachama kadhaa wa kikosi hicho cha RSF. Ripoti hiyo ya Shirika la Amnesty International imesema baadhi ya wanajeshi pia wanatumiwa kwa uhalifu huo.

Jeshi la Sudan limejibu ripoti hiyo kwa kusema limeanzisha kitengo maalum kujaribu kupunguza madhara kwa raia na kwa upande wake kikosi cha RSF kimekanusha madai dhidi ya vikosi vyake kwamba vimehusika na unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vya ukatili katika jimbo la huko Darfur.

Naibu katibu wa Shirika la Amnesty International nchini Ujerumani, Julia Duchrow, amesema kila mahali nchini Sudan, raia wanapitia dhuluma zisizoweza kufikirika wakati ambapo Vikosi vya Msaada wa Haraka na jeshi la Sudan vikiendelea kupigana katika vita vya kudhibiti maeneo.

Kiongozi wa RSF Mohammed Hamdan Daglo. Picha: AFP

Vita vilianza nchini Sudan katikati ya mwezi Aprili kati ya kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na makamu wake Mohammed Hamdan Daglo. Kumekuwa na makubaliano kadhaa ya kusitisha mapigano tangu wakati huo lakini mara kwa mara makubaliano hayo yamekuwa yanakiukwa.

Vyanzo: DPA/AP/AFP