1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty Int: Sera za Trump zimedhoofisha haki za binadamu

Sylvia Mwehozi
22 Februari 2018

Ripoti ya shirika la Amnesty International imesema sera za rais Donald Trump wa Marekani zilirudisha nyuma harakati za haki za binadamu nchini Marekani na duniani kote, lakini zimesaidia kuhamasisha wanaharakati wapya.

Donald Trump bei Wahlkampaqne
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Ehrhardt

Ripoti ya kila mwaka ya shirika hilo, imesema hatua za Trump kuhusu haki za binadamu, zinaweka mfano mbaya kwa mataifa mengine kuiga. Inasema Trump na viongozi wengine wakiwemo rais wa Misri Abdel-Fattah al-Sisi, rais wa Ufilipino Rodrigo Duterte, Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, Rais wa Urusi Vladmir Putin na rais wa China Xi Jinping,  "wanadhoofisha haki za mamilioni".

Katibu mtendaji wa shirika hilo Salil Shetty amesema harakati za wazi za chuki za serikali ya Marekani mwezi Januari 2017 za kupiga marufuku watu kutoka nchi kadhaa zenye waislamu wengi, ziliweka mlolongo wa hatua kwa mwaka ambapo viongozi walizipeleka siasa za chuki katika kiwango cha hatari.

"Uhamasishaji wa chuki na hofu kwa makundi yote ya watu, kwa kuzingatia ni watu wa aina gani, hatimaye unaongoza katika mwelekeo mmoja. Wakati viongozi wanapohimiza au kufunga macho, mwisho wa mchezo unatisha na ni wa kweli," amesema Shetty. 

Mauaji ya watu wa Rohingya pia yagusiwa

Shetty anaongeza kwamba matokeo ya mwisho ya jamii iliyohimizwa chuki yalionekana, kuonea na hofu ya uvamizi wa jamii ya wachache katika kampeni ya kutisha ya safisha safisha ya kikabila dhidi ya watu wa Rohingya nchini Myanmar. Ripoti hiyo inatuhumu jumuiya ya kimataifa kwa kushindwa kushughulikia ripoti za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Myanmar, Iraq, Sudan Kusini, Syria na Yemen.

"Funzo la 2017 ni kwamba hofu na chuki ni kichochea cha ukatili. 2018 unahitaji viongozi wajiandae kukabiliana na changamoto kubwa, kuanzia wakimbizi na kuwalinda watetezi wa haki za binadamu na hali ya hatari ya upatikanaji wa huduma za msingi kwa watu wengi".

Picha ya boti iliyowabeba wakimbizi wanaojaribu kuingia UlayaPicha: Getty Images/M. Bicanski

Ripoti hiyo inasema utawala wa Trump, ulifanya vibaya kuhusu haki za wanawake, kuunga mkono kwa uwazi mateso na kujaribu kuondoa huduma za afya kutoka kwa mamilioni na pia kudhoofisha vyombo vya habari.

Mataifa ya Ulaya na mgogoro wa wahamiaji

Pia ripoti hiyo imewatuhumu viongozi wa mataifa tajiri namna walivyoshugulikia mgogoro wa wakimbizi ikisema viongozi wengi wa Ulaya hawakutaka kukabiliana na changamoto ya wimbi la wakimbizi kwa njia za kisheria, badala yake waliamua kuwa hakuna kitu kinachoweka mipaka katika jitihada za kuwazuia wakimbizi mbali na mipaka yake.

Uchaguzi wa karibuni wa Austria, Ufaransa, Ujerumani na Uholanzi nao uliangaziwa katika ripoti hiyo ambapo baadhi ya wagombea walitaka kutumia wasiwasi wa kijamii na kiuchumi kutia hofu na lawama kama ushahidi wa kwamba "vita vya maadili duniani vimefikia ngazi mpya" mwaka 2017.

Ripoti hiyo pia imezishutumu serikali kwa kutumia usalama wa kitaifa na ugaidi kama kisingizio cha kukandamiza uhuru wa mtu binafsi".

Hata hivyo, Amnesty International imesema iliwezekana kwa "watu wa kawaida" kuchukua hatua, ikitolea mfano wanafunzi wa Florida namna wanavyohimiza udhibiti zaidi wa silaha baada ya mauaji ya hivi karibuni dhidi ya watu kumi na saba, wakiwemo wanafunzi na waalimu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/dpa/afp

Mhariri: Daniel Gakuba

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW