Tanzania yashinikizwa kuelezea aliko Polepole
8 Oktoba 2025
Ripoti iliyotolewa na shirika hilo imeeleza kuwa Serikali ya Tanzania inapaswa kuhakikisha usalama wa Polepole na kuwachukulia hatua za kisheria waliomteka, kwa mujibu wa taratibu za haki na uwazi.
Kulingana na familia ya Polepole, walipokea taarifa ya uvamizi nyumbani kwake eneo la Dar es Salaam asubuhi ya Oktoba 6, 2025. Walipofika, walikuta mlango umevunjwa, nyaya za umeme zimekatwa, na damu nyingi ikiwa imemwagika ndani ya nyumba. Picha na video zilizotolewa na familia zinaonyesha dalili za mapambano makali.
Amnesty: Tuna wasiwasi mkubwa
Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Amnesty International amesema kuwa shirika hilo linapata wasiwasi mkubwa kutokana na taarifa kwamba Humphrey Polepole huenda alitekwa kwa nguvu na kupigwa.
Polepole, ambaye aliwahi kuwa kiongozi mwandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alijiuzulu nafasi yake ya kidiplomasia mapema mwaka huu baada ya kuikosoa hadharani serikali kwa kile alichokiita kupuuzia haki, utawala wa sheria na misingi ya katiba.
Familia ya Polepole iliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Mbezi tarehe 6 Oktoba, huku wakili wake akiwasilisha ombi la kisheria la kuitaka mahakama ikiwa imemuweka kuzuizini kumpeleka mahakamani ili mahakama iweze kuamua.
Familia ya Polepole imeiambia Amnesty International kuwa wakati wa uchunguzi wa polisi, maafisa walichukua baadhi ya vitu kutoka nyumbani kwa Polepole, ikiwemo mashine ya kuchapisha na sanduku la kuhifadhia vitu vya thamani.
Polisi inaendelea na uchunguzi
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime alisema Polepole alitakiwa kufika Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufuatia tuhuma zilizotolewa mitandaoni lakini hakwenda na kusema zinaendelea kuchunguza ukweli wa madai hayo.
Tukio hili linatokea chini ya miezi mitatu tangu Polepole aliripoti kutekwa kwa dada yake kutoka nyumbani kwake Bahari Beach, Dar es Salaam Julai 17, 2025 ambapo taarifa zilieleza kuwa alipigwa na kutelekezwa usiku wa siku iliyofuata.
Kesi hii inaongeza idadi ya matukio ya kutoweka kwa nguvu na mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa serikali nchini Tanzania, jambo linalozua hofu ya kuongezeka kwa ukandamizaji wa kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Jeshi la Polisi lalaumiwa kwa matumizi ya nguvu
Taarifa hio ya Amnesty International imesema kuwa vyombo vya usalama nchini Tanzania vimekuwa vikihusishwa mara kwa mara na matukio ya watu kutoweka kwa nguvu huku kukiwepo watu ambao bado hawajulikani walipo. Miongoni mwao ni pamoja na Anthony Gabriel, Daniel Chonchorio, Deusdedith Soka, Dioniz Kipanya, Fakih Ali Salim, Frank Mbise, Jacob Mlay, Mdude Nyagali, Shadrack Chaula, Sinda Mseti, na Siza Mwita Keheta.
Mnamo Juni 2025, wataalamu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa waliitaka Serikali ya Tanzania kusitisha mara moja matumizi ya mbinu hiyo dhidi ya wapinzani wa kisiasa, watetezi wa haki za binadamu na waandishi wa habari, hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu.