Amnesty International: Mateso ni tatizo la dunia nzima
13 Mei 2014Zaidi ya nusu ya nchi zilizosaini mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mateso miaka 30 iliyopita bado zinawatesa watu. Hayo yamesemwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International katika ripoti yake iliyotolewa leo, likilaani kile lilichokiita kuwa ni mzozo wa kimataifa. Shirika hilo linasema mateso Afrika yameongeza sana huku nchi 10 kati ya 55 barani humo zikiwa zimeridhia sheria inayopiga marufuku mateso.
Serikali kote ulimwenguni zina undumakuwili linapokuja suala la mateso - zimeyapiga marufuku katika sheria lakini zinasaidia kuyafanya," amesema Salil Shetty, katibu mkuu wa shirika la Amnesty International, mjini London Uingereza wakati wa uzinduzi wa kampeni kabambe ya shirika hilo dhidi ya mateso. Tangu mwaka 1984 nchi 155 zimeridhia mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya mateso. Shirika la Amnesty International limefanya utafiti katika nchi 142 na 79 kati ya hizo bado zinatumia mateso. "Huu ni mzozo unaoziathiri tawala za kiimla sawa na zile za kidemokrasia," akaongeza kusema Shetty, wakati wa kutolewa ripoti iliyopewa jina "Mateso mwaka 2014 - Miaka 30 ya ahadi zilizovunjwa".
Shirika hilo limegundua mbinu 27 za mateso zilizotumiwa mwaka jana, zikiwemo matumizi ya vifaa vya umeme, kutobolewa kwa viungo vya wafungwa, ubakaji, kuchomwa kutumia sigara, kuigiza unyongaji, kutengwa kwa muda mrefu na mateso kutumia maji.
Mataifa mengi ya Afrika hayayachukulii mateso kama uhalifu, ingawa mkataba wa Afrika kuhusu haki za binadamu na kiraia unayapiga marufuku. "Serikali za Afrika bado hazijalitambua tatizo hili, ukiacha mbali kuanza kurekebisha hali ilivyo ya mateso," amesema Mkurugenzi wa shirika la Amnesty International barani Afrika, Netsanet Belay. "Ukosefu wa sheria za kitaifa kupiga marufuku mateso katika nchi nyingi za Afrika unaruhusu mateso, sio tu kuendelea kuwepo bali pia kushamiri," akaongeza kusema Belay.
Mataifa ya Afrika yaendelea kufanya mateso
Nchi zisizopungua 24 barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara zimewatesa watu mwaka huu, watafiti wa shirika la Amnesty International wamegundua baada ya kuwahoji watu zaidi ya 21,000 katika nchi 21 duniani kote. Kwa sababu mateso yanayofanywa na dola ni vigumu kuyathibitisha, shirika hilo linakisia takwimu halisi za visa vya mateso kuwa kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa matokeo ya uchunguzi huo, katika nchi nyingi za Afrika matumizi ya mateso na vitendo vingine viovu, vya kikatili na vya kumdhalilisha binadamu ni jambo la kawaida na linakubalika na wengi kama hatua halali ya kuchukua kukabiliana na viwango vikubwa vya uhalifu.
Katika magereza mengi ya Afrika na vituo vya kuwazuia washukiwa mateso hutumiwa mara kwa mara kupata taarifa kutoka kwao, watafiti wamegundua. Wafungwa hutandikwa, kufungwa katika hali za kusababisha uchungu mkali, wakining'inia kutoka kwenye madari ya nyumba na kunyanyaswa kimapenzi nchini Ethiopia, Kenya, Gambia, Mali, Nigeria, Senegal, Sudan na Zimbabwe. Nusu ya Wakenya walioshirikishwa katika utafiti huo nchini Kenya na asilimia 50 nchini Nigeria walisema wana hofu wangekabiliwa na kitisho cha kuteswa watakapotupwa gerezani.
Shirika la Amnesty International lilirekodi visa vya mateso nchini Afrika Kusini, ikiwa ni pamoja na matumizi ya umeme na kipigo cha mbwa katika jela linaloendeshwa kibinafsi na lililo chini ya ulinzi mkali la Mangaung katika jimbo la Free State.
Nchini Mauritania mahakama zilitangaza kwamba kauli za kukiri makosa zinazopatikana kwa njia ya mateso au njia nyingine za unyanyasaji zinakubaliwa kama ushahidi, hata kama baadaye zinafutwa.
Nchini Nigeria, polisi na jeshi hutumia mateso kama jambo la kawaida, kwa mujibu wa shirika la Amnesty. Mateso nchini Sudan hujumuisha matumizi ya kukata viungo kama adhabu. Nchini Liberia shirika la Amnesty limeshuhudia msongamano mkubwa wa wafungwa, ukosefu wa maji safi na uchafu katika magereza, huku vyumba vya mahabusi vikiwa vidogo mno kiasi kwamba wafungwa wanalazimika kupishana kulala kwa zamu.
Mwandishi: Josephat Charo/DPAE/RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel