1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali Uganda yadaiwa kuukandamiza upinzani

5 Januari 2026

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International limevikosoa vyombo vya usalama Uganda kwa kuendeleza ukandamizaji dhidi ya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa Januari 15, 2026.

Uganda Kampala  | Polisi Uganda yadaiwa ´kuwanyanyasa wafuasi wa upinzani
Amnesty International: Serikali Uganda yawanyanyasa wafuasi wa upinzani kuelekea uchaguzi wa Januari 15Picha: Badru Katumba/AFP/Getty Images

Amnesty International imesema imekusanya ushahidi wa kutosha ukionyesha jinsi askari polisi na jeshi waliovyohusika moja kwa moja katika kuwanyanyasa wafuasi na viongozi wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu. Vitendo vya vyombo vya dola kuzuia na kutatiza mikutano ya kampeni za upinzani ambazo zimetambuliwa na tume ya uchaguzi kwa mujibu wa ratiba rasmi ni hali ambayo ilitangulia kudhihirika.

Katika ripoti yake shirika hilo linaelezea kuwa kadri upinzani ulivyojaribu kustahimili hali hii, inasemekana kuwa wafuasi wa upinzani waliendelea kukamatwa na kuzuiliwa. Angalau mtu mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi katika mojawapo ya matukio eneo la Iganga Mashariki mwa Uganda. Tigere Chagutah ambaye ni Mkurugenzi wa Shirika hilo Mashariki na Kusini mwa Afrika amehimiza mamlaka za Uganda kuondokana na mienendo hiyo inayokiuka pakubwa haki za binadamu pamoja na kudoroza demokrasia.

Amnesty: Serikali yaendeleza matukio ya ukandamizaji dhidi ya upinzani

Mamlaka za dola zimendeleza matukio ya kukandamiza upinzani na wafuasi wao, hali ambayo inawatatiza kutelekeza haki na uhuru wao wa kutangamana.Ni lazima mamlaka zidumishe dhima ya kulinda haki za binadamu na kuepukana na ukandamizaji wa upinzani ambapo viongozi na wafuasi wao wamekamatwa na kuzuiliwa huku wengine wakiteswa kimwili.

Nembo ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty InternationalPicha: Pond5 Images/IMAGO

Watu mbalimbali walioshuhudia visa hivyo katika vitongoji vya Kampala ikiwemo Kawempe walielezea jinsi wanajeshi wanavyoziba barabara na kuwatawanya wafuasi wanaomsindikiza mgombea. Mengi ya matukio haya yamekumba chama kikuu cha upinzani NUP ambacho mgombea wake Robert Kyagulanyi ndiye amedhihirisha ushindani mkubwa dhidi ya rais Yoweri Museveni ambaye aliingia madarakani takribani miaka 40 baada ya kupigana vita vya uasi kupinga matokeo ya uchaguzi ya mwaka 1980.

Zaidi ya wat 400 wamekamatwa na serikali ya Museveni

Kulingana na ripoti ya Amnesty zaidi ya watu 400 wamekamatwa katika kipindi cha kampeni, miongoni mwao wakiwa wagombea ubunge na maafisa wa ngazi za juu wa NUP. Baadhi ya wanaharakati wa haki za binadamu wameunga mkono ripoti hiyo ya Amnesty wakiongezea kuwa kukamatwa

Amnesty yasema zaidi ya watu 400 wamekamatwa katika kipindi cha kampeni, miongoni mwao wakiwa wagombea ubunge na maafisa wa ngazi za juu wa NUP. Picha: Dai Kurokawa/dpa/picture alliance

kwa mwenzao Sarah Birete ambaye mahakama ilimnyima dhamana hadi baada ya uchaguzi mkuu tarehe 21 ni kielelezo kuwa haka wao wanaandamwa na vyombo vya dola.

Ijapokuwa hadi wakati wa kuandaa taarifa hii, mamlaka za Uganda zilikuwa hazijatoa tamko rasmi kuhusu ripoti ya Amnesty, wasemaji wa polisi na jeshi na hata maafisa wa ngazi za juu katika jeshi wamendelea kusisitiza kuwa madai ya upinzani kunyanyaswa yanaegemea tu upande mmoja bila kuchunguza kwamba hata wakati mwingine wafuasi wao ndiyo hutangulia kuchokoza vyombo hivyo.

Katika hali ya askari hao kujilinda, wanafyatua risasi na mabomu ya kutoa machozi na kwa bahati mbaya maafa na majehara hutokea. Zikiwa zimesalia siku 8 za wagombea kusaka kura, wiki hii rais Museveni atafanya kampeni zake mjini Kampala na ulinzi umeimarishwa katika mitaa na barabara za mji huo.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW