1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wengi nchini Somalia waendelea kuyakimbia makazi yao

Zainab Aziz Mhariri: Josephat Charo
21 Julai 2020

Amnesty International imesema watu nchini Somalia wanayakimbia makaazi yao ili kuepuka dhiki inayosababishwa na mapigano,ukame pamoja na janga la nzige lisilokuwa na kifani katika kipindi cha miaka 25 iliyopita.

Somalia Explosion einer Autobombe in Mogadischu
Picha: picture-alliance/AP/F.A. Warsameh

Shirika hilo limesema katika ripoti yake kwamba, wakimbizi wa ndani nchini Somalia wanakabiliana na dhiki hizo katika muktadha wa janga la maambukizi ya corona. Kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya afya, hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita watu wapatao 3,119 walikuwa wameambukizwa virusi vya corona na nusu ya hao katika jimbo la Banadir karibu na mji mkuu, Mogadishu. Kwa sasa wapo wakimbizi wa ndani wapatao nusu milioni kwenye jimbo hilo.

Mkurugenzi wa Shirika la Amnesty International kanda ya Mashiriki na kusini mwa Afrika Deprose Muchena ameeleza kwamba idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani nchini Somalia wanaishi katika sehemu zilizojazana, ambapo huduma za afya ni hafifu na hakuna maji safi wala mazingira siyo safi.

Wakimbizi wa ndani nchini Somalia wanakabiliwa na hatari ya kufukuzwa kwenye makaazi yao wakati  ambapo hawana ajira. Naibu mkurugenzi wa shirika la haki za binadamu la Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki Seif Magango ameeleza juu ya hali inayowasibu wakimbizi hao wa ndani.

Janga la nzigePicha: picture-alliance/AP Images/B. Curtis

Shirika la Amnesty International limesema serikali ya Somalia na washirika wa kimataifa wahakikishe kwamba wakimbizi wa ndani wanapewa haki ya kupata huduma ya maji safi, afya na makazi bora, kulingana na haki za binadamu kwa viwango vya kimataifa katika kupambana na maambukzi ya virusi vya corona.

Wakaazi waliohojiwa na Amnesty International kwenye kambi zao wamethibitisha kwamba huduma za afya wanazopatiwa ni hafifu sana na kwamba hakuna zoezi la kuwapima watu ili kubaini kama wameambukizwa  virusi vya corona.

Wafanyakazi wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayowasaidia wakimbizi wa ndani kwenye kambi za Kahda, Weydow na Daynile nchini Somalia wamesema kupungua kwa huduma za afya kumesababishwa na ukosefu wa fedha na kutokana na amri zilizowekwa kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona. 

Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Mashariki na kusini mwa Afrika Deprose Muchena ameishauri serikali ya Somalia kuomba msaada wa kimataifa ili kuweza kuwahudumia vizuri wakimbizi wa ndani nchini humo. 

Chanzo: Amnesty International