1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International:Janga la Covid linatumiwa kubinya haki

Saleh Mwanamilongo7 Aprili 2021

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International iliotolewa leo inaelezea kuhusu madhila ya janga la Covid-19 kwa walio wachache, wahudumu wa afya na wanawake katika nchi kadhaa duniani.

Uganda Johannesburg  Coronavirus Maßnahmen Polizei
Picha: Getty Images/AFP/B. Katumba

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International iliotolewa leo inaelezea kuhusu madhila ya janga la Covid-19 kwa walio wachache, wahudumu wa afya na wanawake katika nchi kadhaa duniani. Ripoti hiyo inaelezea kwamba janga la Covid-19 linatumiwa na viongozi katika kubinya haki za binadamu. Mkuu mpya wa shirika hilo Agnes Callamard, ametoa mwito kwa ajili ya kurekebishwa kwa mifumo kadhaa iliochakaa,ukiwemo mfumo wa afya. 

 Ripoti hiyo ya mwaka 2020 na 2021 ya shirika la Amnesty International inaangazia haki za binadamu katika nchi 149 kote duniani. Kwenye ripoti hiyo, shirika la Amnesty linasema kuwa raia ambao tayari walikuwa wameathirika na kutengwa na uongozi wakiwemo wanawake na wakimbizi ndio walioathirika sana na janga hili la Covid-19.

Soma zaidi:Amnesty yashutumu mauaji ya raia mzozo wa Msumbiji

 Wahudumu wa afya,wafanyakazi wahamiaji na watu wanaofanya kazi kwenye sekta ya biashara rejareja na ambao wengi wao walikuwa kwenye mustari wa mbele katika kupambana na corona,walifadhahishwa pia na mfumo wa afya uliochakaa na misaada ya kiutu ya kusuasua.

Hatua za vizuwizi zilizochukuliwa na baadhi ya viongozi zilichangia pia kubinya haki za binadamu,linaelezea shirika la Amnesty International.

Amnesty International imesema janga la Covid-19 limevuruga huduma za idara ya umma

Polisi ya Kenya ikiwaamuru abiria kulala chini karibu na kivuko cha Likoni, MombasaPicha: picture-alliance/AP Photo

Agnes Callamard, mkuu mpya wa shirika la Amnesty International amesema kuwa janga la Covid-19 liliongeza tofauti na kuvuruga huduma za idara za umma.

Ripoti hiyo inaonyesha pia mpasuko wa miongo kadhaa ya uongozi mbaya dhidi ya waliowachache,wakimbizi, wazee na wanawake katika kipindi cha janga la Covid-19.

Shirika la Amnesty International, limetoa mfano wa Uganda ,nchi ambayo inawapokea wakimbizi milioni 1.4, ilifunga mipaka yake mara lilipozuka janga la Corona bila kutofautisha wakimbizi na watu wanao omba hifadhi waliotaka kuingia nchini humo. Kinyume cha hatua hiyo ni kwamba zaidi ya watu elfu kumi walizuwiliwa kwenye mpaka baina ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Nchini Tanzania, serikali ili bana vyombo vya habari,ikielezea kwamba vinasambaza uvumi kuhusu janga la Covid-19, huku mwezi Juni, aliekuwa rais wake John Magufuli akitangaza kuwa Tanzania haina corona. Vyombo vya habari vilifungwa kwa sababu ya kutangaza taarifa za upinzani.

Polisi nchini Kenya,walitumia nguvu ya kuzidi kiasi,iliyosababisha hadi mauwaji, kwa ajili ya kuheshimisha hatua ya vizuwizi vilivyo wekwa.

 Kupigwa,kutoweka na kamatakamata ya wapinzani ama wafuasi wao vilishuhudiwa pia nchini Burundi na shirika la Amnesty International mnamo kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Nchini Rwanda, shirika la Amsety International linasema visa vya kesi zisizo za haki na huru,kukamtwa kinyume cha sheria na matumizi ya nguvu ya kupindukia kiasi viliendelea nchini humo.

Na huko Nchini Congo, mauwaji ya raia yanaendelea kwenye majimbo ya Kivu, huku wanaharakati wa haki za binadamu wakitishiwa maisha yao. Inaelezea ripoti hiyo ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International.