1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yailaumu Kenya uvunjifu haki za binaadamu

13 Julai 2023

Shirika la haki za binaadamu la Amnesty International limechapisha ripoti inayolezea jinsi vyombo vya dola vinavyokiuka haki za binaadamu nchini Kenya wakati maandamano ya upinzani yakiendelea kushinikiza nafuu ya maisha

Themenpaket | Kenia Proteste Regierung Wirtschaft
Picha: Samson Otieno/AP/picture alliance

Mashirika ya kimataifa ya haki za binaadamu - Amnesty International na Civicus -  yamechapisha ripoti kuhusu taswira ya haki za binaadamu nchini Kenya.

Ripoti hiyo inasema kuwa matumizi ya nguvu kupita kiasi, udhalilishaji na kutiwa mbaroni kwa waandamanaji na wanahabari wakati wa maandamano ni baadhi ya ukiukwaji wa haki za raia unaofanywa na vyombo vya dola.  

"Mara nyingi nchini Kenya haki ya kimsingi ya kukusanyika kwa amani na kujieleza huambatana na hatari ya vurugu na hata maafa," alisema Sylvia Mbataru, afisa wa shirika la Civicus.

Soma zaidi: Maandamano ya upinzani yaendelea kuiandama Kenya

"Hatuwezi kusamehewa kama taifa, lazima tujitahidi kupunguza mapengo haya, unapoangalia umaskini wakati wa janga UVIKO-19, ulifanywa kuwa hatia, watu waliotafuta chakula walitiwa nguvuni." Aliongeza afisa huyo.

Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Kulingana na ripoti hiyo kwa jina "Kitisho dhidi ya mamlaka ya wananchi mwaka 2022," sheria kali, kubinya uhuru wa vyombo vya habari, vitisho, kukamatwa na kuzuiliwa kwa wanahabari na zile zinazopinga maandamano ni miongoni mwa haki kumi za binadamu zinazokiukwa nchini Kenya.

Gachagua alaani uharibifu wa mali kwenye maandamano

Kwa upande mwengine, Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amekosowa vikali kile alichosema ni uharibifu unaofanywa na waandamanaji nchini humo.

Akizungumza jijini Nairobi siku ya Alkhamis (Julai 13) wakati wa uzinduzi wa mkutano wa bunge juu ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Gachagua alisema kuwa anasikitishwa na maafa pamoja na uharibifu wa mali katika pembe mbali mbali za taifa, baada ya upinzani pamoja na wamiliki wa magari ya uchukuzi wa abiria kufanya maandamano.

Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Soma zaidi: Watu 6 wauawa katika maandamano ya upinzani Kenya

Watu 600 wametiwa nguvuni na wanazuiliwa katika vituo mbali mbali vya polisi.

Ripoti zinadai kuwa watu 10 walipoteza maisha kwenye maandamano hayo kwa kupigwa risasi na maafisa wa polisi kwenye kaunti 30 kati ya 47 zilizofanya maandamano. 

Gachagua aliwataka viongozi "kutimiza ahadi walizotoa kwa wapiga kura", badala ya kujihusisha na kile alichosema kuwa ni mambo yasiyo na msingi.

Kenya yapoteza shilingi bilioni 3 kwa maandamano

Hayo yanajiri Chama cha Wafanyibiashara nchini Kenya (KEPSA) kilisema kuwa taifa lilipoteza mali ya thamani ya shilingi bilioni tatu za Kikenya.

Picha: THOMAS MUKOYA/REUTERS

Mbali na maandamano hayo, usafiri ulisitishwa pembe zote za taifa huku wamiliki wa magari ya uchukuzi wa abiria wakipinga hatua mpya za serikali za kuwarejesha madereva wote darasani kutokana na kuongezeka kwa visa vya ajali za barabarani.

Soma zaidi: Polisi Kenya yatumia gesi ya machozi kutawanya waandamanaji

Waziri wa Usalama wa Taifa, Kithure Kindiki, alionya kuwa wahusika wote wa maandamano wangelichukuliwa hatua za kisheria.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Kindiki alisema wote waliohusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja wangelikabiliwa na mkono mrefu wa sheria.

Imetayarishwa na Shisia Wasilwa/DW Nairobi