1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yalaumiwa kwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
23 Julai 2021

Mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch yamesema Iran imetumia nguvu kupindukia dhidi ya waandamanaji wanaolalamika juu ya uhaba wa maji katika jimbo la Khuzestan.

Kombobild Irans neuer Präsident Ebrahim Raisi und Logo der Organisation Amnesty International

Amnesty International imesema vikosi vya usalama vya Iran vimefyatua risasi za moto ili kuzima maandamano ya amani na kwamba mpaka sasa shirika hilo limethibitisha vifo vya waandamanaji wasiopungua wanane akiwemo barobaro mmoja. Diana Eltahawy, naibu mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini amelaani matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji. 

Kiongozi Mkuu wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: Iranian Leader Press Office/AA/picture alliance

Eltahawy amesema raia wa Khuzestan bado wana wanakumbuka yaliyotokea mwezi Novemba mwaka 2019 yalipofanyika maandamano ya kitaifa kupinga kuongezeka bei ya mafuta ambapo, kulingana na Amnesty International watu wapatao 304 walifariki kutokana na vurugu zilizotokea wakati maafisa wa usalama walipokuwa wanajaribu kuyazima maandamano hayo.

Nalo shirika la kimataifa la Haki za Binadamu Human Rights Watch limesema katika taarifa tofauti kwamba mamlaka ya Iran imetumia nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji na hivyo serikali inapaswa kuchunguza kwa uwazi vifo vyote vilivyoripotiwa.

Rais anayeondoka wa Iran Hassan Rouhani Picha: Iranian Presidency/Zuma/imago images

Mtafiti wa Human Rights Watch nchini Iran Tara Sepehri Far amesema vikosi vya usalama vya serikali  vinajulikana kwa visa vya kutumia risasi za moto dhidi ya waandamanaji ambao huwa wanaandamana kwa sababu huwa wamefadhaishwa na kuongezeka kwa matatizo ya kiuchumi na kuzorota kwa hali yao ya maisha.

Wakati huo huo kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema anaelewa hasira za waandamanaji kuhusiana na ukame katika eneo hilo la kusini magharibi mwa nchi hiyo. Tamko la kiongozi huyo mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei aliyezungumza kupitia televisheni ya taifa likiwa ni la kwanza la moja kwa moja kutoka kwake juu ya maandamano hayo tangu yalipoanza wiki iliyopita katika jimbo la Khuzestan.

Rais mpya wa Iran Ebrahim RaisiPicha: Vahid Salemi/AP Photo/picture alliance

Kiongozi wa kidini wa Iran amesema ni sawa watu kuonyesha kutoridhika kwao, lakini wanapaswa kufahamu kuwa swala la matatizo ya upatikanaji maji katika eneo la Khuzestan linalokabiliwa na joto kali na ukame sio swala dogo. Khamenei amewahimiza wakaazi wa eneo hilo lililokumbwa na ukame la kusini magharibi kutowapa maadui wa Iran nafasi ya kuivuruga nchi.

Vyanzo:AP/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW