1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty International yalaani uhalifu wa kivita Afghanistan

15 Desemba 2021

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International limetoa ripoti yake inayoelezea uhalifu wa kivita na ukatili uliofanywa nchini Afghanistan katika mapigano yaliyoendeshwa na kundi la Taliban.

Afghanistan Taliban Tötungen Symbolbild
Picha: WAKIL KOHSAR AFP via Getty Images

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Jumatano, kundi la Taliban, jeshi la Marekani na vikosi vya usalama vya Afghanistan vyote vilihusika na mashambulizi yaliyosababisha mateso makubwa kwa raia wakati Taliban ilipochukua madaraka na kuindoa serikali iliyokuwa ikitambuliwa kimataifa. 

Ripoti hiyo inaangazia mateso na mauaji holela yaliyofanywa na Taliban wakati wa hatua za mwisho za mzozo wa Afghanistan, pamoja na vifo vya raia wakati wa mfululizo wa operesheni za anga na ardhini zilizofanywa na jeshi la ulinzi la Afghanistan na vikosi vya usalama vya nchi hiyo, ANDSF pamoja na vikosi vya jeshi la Marekani.

Nyumba ziligeuzwa maeneo ya uhalifu

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnes Callamard amesema nyumba, hospitali, shule na maduka ziligeuzwa kuwa maeneo ya uhalifu ambapo watu waliuawa na kujeruhiwa mara kwa mara. Callamard ameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC kuchunguza uhalifu wote wa kivita ambao unawezekana kufanywa, bila kujali utaelekea wapi.

Katika ripoti hiyo Taliban inashutumiwa kwa kuwatesa na kuwaua watu wa dini na makabila ya wachache pamoja na waliokuwa askari wa vikosi vya usalama vya Afghanistan, wakati wa kuitwaa miji mipya. Waathiriwa walizungumzia ukatili uliofanywa na wanamgambo katika wilaya zipatazo mbili kwenye jimbo la Panjshir, pamoja na eneo la Spin Boldak kwenye jimbo la Kandahar.

Ripoti ya Amnesty International inaeleza kuwa takriban watu sita waliuawa katika kijiji cha Panjshir kwa kupigwa risasi kichwani, kifuani au kwenye moyo na kwamba mauaji ya aina hiyo ni sawa na uhalifu wa kivita. Ripoti hiyo pia inazungumzia mashambulizi manne ya anga yaliyofanywa na vikosi vya anga vya Marekani na Afghanistan katika miaka ya hivi karibuni na kuwaua jumla ya raia 28 na kuwajeruhi wengine sita.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Agnes Callamard Picha: Claudio Bresciani/TT News Agency/picture alliance

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema kuna ''madai ya kuaminika'' kuhusu mauaji holela ya zaidi ya watu 100 nchini Afghanistan yaliyofanywa tangu Taliban ilipochukua madaraka mwezi Agosti. Naibu kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Nada Al-Nashif siku ya Jumanne aliliambia Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwamba anasikitishwa sana na taarifa za kuendelea kwa mauaji kama hayo, licha ya msamaha wa jumla kutangazwa na Taliban baada ya kuchukua madaraka Agosti 15.

''Kati ya Agosti na Novemba, tumepokea madai ya kuaminika ya mauaji ya zaidi ya askari 100 wa zamani wa vikosi vya usalama vya Afghanistan na wengine wanaohusishwa na serikali iliyopita, huku mauaji ya watu wapatao 75 yakidaiwa kufanywa na Taliban'', alisema Al-Nashif.

Miili ilionyeshwa hadharani

Al-Nashif anasema katika matukio kadhaa, miili ilionyeshwa hadharani na kwamba hali hiyo imezidisha hofu miongoni mwa jamii. Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan umeripoti kwamba raia 1,659 waliuawa na wengine 3,524 walijeruhiwa katika miezi ya kwanza ya mwaka huu wa 2021, idadi hiyo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 47 ikilinganishwa na mwaka uliopita wa 2020.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya serikali ya Taliban, Abdul Qahar Balkhi amesema serikali yake imejizatiti kikamilifu kuzingatia amri ya msamaha na amekanusha madai kwamba wafanyakazi wa serikali iliyopita walikuwa wakiteswa.

''Mtu yeyote atakayekutwa anakiuka amri ya msamaha atafunguliwa mashtaka na kuadhibiwa'', alifafanua Balkhi. Wizara hiyo imesema matukio yatachunguzwa kwa undani, lakini uvumi usio na uthibitisho haupaswi kuchukuliwa kwa thamani.

Shirika la Amnesty International limezitolea wito kundi na Taliban na serikali ya Marekani kutimiza wajibu wao wa kimataifa na kuanzisha mifumo iliyo wazi na thabiti kwa raia kuomba fidia kutokana na madhara waliyoyapata wakati wa vita.

 

(DPA, AFP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW