1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yamtaka rais Tshisekedi kutekeleza ahadi yake

Saleh Mwanamilongo
17 Juni 2020

Shirika la Amnesty International limemtuhumu Rais Felix Tshisekedi kutotekeleza ahadi yake ya kuwatendea haki wahanga wa visa vya ukiukaji wa haki za binadamu.

Maafisa wa polisi kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi CENI,jijini Kinshasa ,kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi.
Maafisa wa polisi kwenye makao makuu ya tume ya uchaguzi CENI,jijini Kinshasa ,kabla ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi.Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Delay

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limemtuhumu Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Felix Tshisekedi kutotekeleza ahadi yake ya kuwatendea haki wahanga wa visa vya ukiukaji wa haki za binadamu chini ya utawala wa mtangulizi wake Joseph Kabila. Kwenye ripoti yake shirika hilo linaelezea kwamba hadi sasa rais Tshisekedi hajaamuru uchunguzu wa mauwaji ya zaidi ya watu 320 kufuatia machafuko ya kabla ya uchaguzi nchini Kongo.

Kwenye ripoti yake inayoitwa ''Bila Maendelezo'' shirika la Amnesty International limesema Rais Tshisekedi, wakati huo akiwa mpinzani, ameshindwa kutekeleza ahadi aliotoa kwa familia za wahanga wa machafuko ya kabla ya uchaguzi,alisema Jean-Mobert Senga,mtafiti wa shirika la Amnesty International kwa ajili ya Kongo.

''Tunamtuhumu rais Tshisekedi kwa sababu ni mwaka mmoja na nusu toka achukuwe madaraka hakuna chochote ambacho kimefanyika.Tumemuomba kutenda sasa kwa sababu kikatiba anamamlaka,ya kuwahakikisha wahanga wanatendewa haki''.

Shirika hilo limeorodhesha zaidi ya vifo 320 mnamo kipindi cha mwaka 2015 hadi 2018 kutokana na maandamano ya kupinga kuweko na muhula wa tatu wa rais wa wakati ule Joseph Kabila.

Maandamano yakuomba kuitishwa kwa uchaguzi wa rais wa mwaka 2018. Picha: Getty Images/AFP/E. Soteras

Kelly Tshimanga, mtoto wa mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu, Rossy Mukendi ameiambia Amnesty Internationak kwamba Tshisekedi wakati akiwa bado mpinzani aliwatembelea nyumbani na kuwaahidi kwamba ''atakuwa kwa ajili yao'', lakini toka achukuwe madaraka hajaonyesha ishara yoyote. Mukendi aliuawa kwa kupigwa risasi mjini Kinshasa tarehe 25 Februari 2018, baada ya kutokea maandamano yaliyoitishwa na Kanisa Katoliki nchini humo.

Hali ya kibinadamu bado haijaimarika

Shirika la Amnesty International limelezea kwamba licha ya matumaini makubwa ya raia wa Kongo kuhusu mageuzi ya kisiasa yaliotokea kufuatia uchaguzi wa mwaka 2018, lakini hali ya kibinadamu bado haijaimarika. 

''Watu wanaendelea kuuawa Ituri, Beni, Kivu ya Kusini na kwengineko. Kwa ujumla hali ya haki za binadamu nchini Kongo ni mbovu na inaendelea kuharibika kutokana na ugonjwa huu wa Covid-19'' alisema Senga.

Shirika la Amnesty International limemuomba Rais Tshisekedi na serikali yake kuhakikisha wazi kwamba wahusika wa ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Alipochukuwa madaraka, Rais Tshisekedi aliruhusu kurejea kwa wapinzani waliokuwa uhamishoni, akiwemo Moise Katumbi na kuachiwa huru kwa wafungwa kadhaa wa kisiasa na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu.