1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty Intl: Navalny sio mfungwa mwenye dhamira ya dhati

Sylvia Mwehozi
24 Februari 2021

Shirika la Amnesty International limesema halimtambui tena kiongozi wa upinzani wa Urusi anayetumikia kifungo jela Alexai Navalny kama mfungwa mwenye dhamira njema kutokana na kauli za chuki alizotoa kipindi cha nyuma

Russland | Moskau | Russischer Oppositionspolitiker Alexej Nawalny vor Gericht
Picha: Alexander Zemlianichenko/AP Photo/picture alliance

Kukamatwa kwa mwanasiasa huyo wa upinzani katika uwanja wa ndege mnamo mwezi Januari, kulichochea miito kutoka makundi ya haki za binadamu nchini Urusi na nje ya nchini pamoja na viongozi wa nchi za magharibi, wanaotarajiwa kuiwekea vikwazo Moscow kutokana na hatua hiyo.

Lakini Amnesty International imesema imechukua uamuzi wa kubatilisha hadhi ya kumtambua Navalny kama mfungwa mwenye dhamira ya kweli kutokana na kauli alizoitoa kipindi cha nyuma. Ingawa shirika hilo halikutaja moja kwa moja kauli aliyowahi kuitoa Navalny lakini kiongozi huyo amewahi kunukuliwa mwanzoni mwa taaluma yake ya kisiasa muongo mmoja uliopita akichochea ukosoaji na kauli za kupinga wahamiaji.

Wiki iliyopita shirika hilo liliwasilisha saini 200,000 kwa mamlaka za Urusi zinazotaka kuachiwa haraka kwa Navalny. Timu ya kiongozi huyo ilijibu mara moja uamuzi wa shirika hilo, ikilituhumu kundi hilo kuegemea kampeni inayoendeshwa na mwandishi wa habari anayehusishwa na vyombo vya habari vya serikali ya Urusi.

Purukushani ya polisi na waandamanaji MoscowPicha: Peter Kovalev/dpa/TASS/picture alliance

Mshirika wa karibu wa kiongozi huyo Leonid Volkov aliandika katika ukurasa wa Twitter kwamba Amnesty na uamuzi wake huo imetangaza kulishwa ujinga wakati mshirika mwingine Ivan Zhdanov naye akiandika kwamba uamuzi huo "ulikuwa wa aibu kubwa".

Jumatatu wiki hii waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas aliwaeleza mawaziri wenzake wa Ulaya wa kuidhinisha vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi waliohusika kumfunga Navaly na ukandamizaji dhidi ya wanaharakati.

"Tayari tuliweka wazi wakati kiongozi wa upinzani akikamatwa kwamba hatukubali ukiukwaji huu wa sheria za kimataifa na tumeweka vikwazo. Na tutakubaliana ikiwa tutapeana mamlaka hapa Brussels ya kuiwekea tena vikwazo Urusi, haswa kwasababu ya hukumu ya Navalny. Ukweli kwamba sasa anatakiwa kutumikia kifungo chake gerezani hilo litatutia wasiwasi leo".

Hayo yakijiri, rais wa Urusi Vladmir Putin leo ameidhinisha sheria zinazoongeza faini ya makosa yaliyotendwa wakati wa maandamano ya kumuunga mkono kiongozi huyo wa upinzani, ambapo maelfu ya watu walikamatwa. Sheria hizo zimeongeza faini sambamba na siku 15 za kukaa mahabusu. Sheria hiyo iliyofanyiwa marekebisho pia imeanzisha faini kwa waratibu wa maandamano ambao wanakiuka kanuni za ufadhili.

Polisi waliwakamata watu zaidi ya 11,000 katika maandamano ya nchi nzima mapema mwaka huu waliokuwa wakimuunga mkono Navalny. Wizara ya mambo ya ndani ilionya awali kuwa itavunja mikusanyiko yote isiyo halali na wale watakaoshiriki wataandamwa na mkono wa sheria. Washirika wa Navalny wengi wao hivi sasa wamekimbia nje ya nchi ama wako chini ya kifungo cha nyumbani.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW