COP29: Mataifa tajiri yakamilishe ahadi ya fedha
4 Novemba 2024Mwito huo umetolewa wakati ambapo mabadiliko ya hali ya hewa yanawalazimisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao barani Afrika.
Shirika hilo la kutetea haki za binadamu pia limeyataka mataifa hayo tajiri kuzifadhili kikamilifu serikali za mataifa ya Afrika ili kuzuia kuhamishwa kwa lazima kwa watu, kusitisha ukiukwaji wa haki za binadamu na kuzisaidia nchi hizo kuacha kwa haraka uzalishaji na matumizi ya nishati ya visukuku.
Amnesty inasema kufikia sasa, mataifa hayo tajiri duniani yameahidi kutoa chini ya dola milioni 700 kati ya zile dola bilioni 400 ambazo nchi maskini zinakadiria kuhitaji kwa ajili ya hasara na uharibifu ifikiapo mwaka 2030.
Soma pia:Papua New Guinea yatangaza kususia mkutano wa COP29
Utafiti wa Amnesty unaonyesha kwamba katika kila pembe ya bara la Afrika, ukame, mafuriko au joto ni mambo yanayowapelekea watu kuyahama makaazi yao katika nchi tofauti na hata kuvuka mipaka hilo likisababisha ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo ukosefu wa makaazi, ukosefu wa chakula, huduma za afya pamoja na hatari ya unyanyasaji wa kijinsia na hata kutokea kwa vifo.
Amnesty inasema licha ya kuwa serikali za Afrika zenyewe zina jukumu la kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa katika mgogoro huu, haziwezi kufanya hivyo bila kupewa ufadhili na nchi tajiri.
Nchini Sonalia pekee, zaidi ya watu milioni moja wameyahama makaazi yao kutokana na ukame na mafuriko ya kila mara ambayo yameharibu mashamba kuwauwa mifugo na kuharibu majumba na kuzipelekea jamii ambazo tayari zimekuwa katika hali ngumu ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, kukimbilia kambi za wakimbizi nchini Kenya au Ethiopia.
Kuongezeka kwa kina cha bahari
Katika pwani ya Senegal kiwango cha maji ya bahari kinachoongezeka kimeviharibu kabisa vijiji na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia na kutafuta makaazi kwengineko.
Nchini Chad nako, ongezeko la joto limezisukuma jamii za wafugaji kusini mwa nchi hiyo kuliko na wakulima, jambo lililosababisha mapigano makali kati ya jamii hizo mbili kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri wa mizozo na uungwaji mkono wa makundi yote mawili.
Sehemu nyingi za bara la Afrika zinakabiliwa na ukame mbaya sana, hali ambayo huenda ikawa imezidishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Soma pia:Viongozi wa ngazi za juu wawasili kwenye mkutano wa mazingira
Ukame wa miaka sita nchini Madagascar umewalazimisha zaidi ya watu 56,000 wa jamii ya Antandroy kuziacha ardhi za mababu zao na kutafuta maeneo mengine ya kuishi na huko wanakabiliwa na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Wakati huo huo, kusini mwa Afrika, ukame mkali uliofuatana umewasukuma watu ukingoni.
Nchini Angola, njaa imesababisha wanawake na watoto kuhamia Namibia kutafuta chakula, hatua inayoongeza hatari ya unyanyasaji, ulanguzi, unyanyasaji wa kijinsia na kutatizwa kwa elimu.
Kutokana na yote hayo na mengine mengi, Amnesty inasema nchi zinazohusika na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi pamoja na taasisi za kifedha za kimataifa, zinastahili kuchukua jukumu na kuhakikisha kwamba raslimali zinazohitajika zinawafikia waathirika.