1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Raia lazima walindwe Kongo

22 Juni 2022

Ripoti ya Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty imesema pande zinazopigana lazima zihakikishe kwamba raia wanalindwa wakati wa mapigano kati ya kundi la waasi la M23 na jeshi la Kongo.

DR Kongo Flüchtlinge
Picha: AFP via Getty Images

Mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yamesababisha vifo vya raia 23 tangu Mei 2022, wakiwemo watoto watatu kulingana na Umoja wa Mataifa.

soma Wakuu wa Afrika Mashariki wakubali kupeleka jeshi, DRC

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa shirika la Amnesty tawi la Mashariki na Kusini mwa Afrika  Deprose Muchena, Kuongezeka kwa jeshi mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemkrasia ya Congo tangu kuibuka tena kwa M23 kunaleta matokeo mabaya kwa raia.

Muchena amezitaka pande zote zinazohusika kwenye mzozo  ziheshimu kikamilifu sheria za kimataifa na kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zote  ili kuhakikisha usalama wa raia.

soma Wakongo na mashirika ya kiraia waliunga mkono jeshi

Tangu kuzuka upya kwa waasi wa M23 mnamo Novemba 2021, mvutano umeongezeka kati ya serikali za Kongo na Rwanda. Katika siku za hivi karibuni, kumeendelea hali ya kushambuliana kwa maneno makali na kimwili yanayolenga watu waliotajwa kama Wanyarwanda au Watutsi mitandaoni nchini Jamuhuri ya Kidemkrasia ya Kongo.

Mamlaka ya Kongo, Umoja wa Mataifa na taasisi kadhaa nchini ndani na nje ya Kongo zimeshutumu vikali uchochezi wa chuki.

Ghasia zimeongezeka

Picha: Moses Sawasawa/AP/picture alliance

Kulingana na shirika linalofuatilia masuala ya usalama katika eneo la kivu-Kivu Security Tracker  eneo la mashariki mwa Kongo limekumbwa na vita tangu miaka ya 1990 na ghasia zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, huku zaidi ya raia 7,380 wakiuawa kati ya 2017 na Aprili 2022.

Rais Félix Tshisekedi alitangaza hali ya hatari huko Kivu Kaskazini tangu Mei 2021 katika jaribio la kupunguza ghasia. Badala yake, ukosefu wa usalama umeongezeka na shirika la Amnesty liligundua kuwa mamlaka imetumia hali ya hatari kuzuia uhuru wa kujieleza na kukusanyika kwa amani, na kutekeleza ukiukaji mwingine wa haki za binadamu bila kuadhibiwa.

Serikali ya Jamuhuri ya Kidemkrasia ya Kongo inaishutumu Rwanda kwa uchokozi ikitumia M23 kama wakala, na spika wa Bunge la Kongo alinukuliwa na vyombo vya habari akishutumu Uganda kwa  kushirikiana na waasi M23 na Rwanda wakati wa vita vya Bunagana vya Kivu Kaskazini tarehe 13 Juni 2022. 

soma DRC yadai askrai 500 wa Rwanda wameingia nchini mwake

Kinyume chake, Rwanda inaishutumu Kongo kwa uchokozi na kushirikiana na waasi wa Wakihutu wa Rwanda FDLR kwa kuendesha harakati zake mashariki mwa Kongo, kundi la  wanamgambo wa Uganda la Interahamwe na wanajeshi wa zamani wa Rwanda waliohusika na mauaji ya kimbari ya Rwanda mwaka 1994 pamoja na wapiganaji ambao hawakuhusika katika mauaji ya halaiki, wakiwemo vijana.

Haya yanajiri siku moja tu baada ya Wakuu wa mataifa ya Afrika Mashariki kukubaliana kupeleka jeshi la kikanda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kumaliza vita mashariki mwa nchi hiyo na kutoa mwito wa kusimamishwa mapigano mara moja.

 

Chanzo/Amnesty International

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW