1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Ulaya iache kuiuzia silaha Misri

Admin.WagnerD25 Mei 2016

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limetoa wito kwa Umoja wa Ulaya kuacha mara moja mauzo ya silaha kwa Misri kutokana rekodi za ukiukaji wa haki za binaadamu kwa kuwa zinachochea mauwaji.

Ägypten Proteste für Demokratie 2013 Tote
Maandamano ya 2013 nchini Misri, watu 200 waliuwawa na wengine 4,500 kujeruhiwa katika uwanja wa Rab'a Al-AdaweyaPicha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Elshamy

Katika taarifa mpya ya Amnesty inaeleza takribani nusu ya mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya yamekiuka hatua ya usimamishaji wa kupeleka silaha nchini Misri na hivyo kusababisha hatari mbaya ya wimbi la mauwaji holela, watu kutoweshwa na mateso.

Mmoja wa maafisi wa Amnesty, Magdalena Mughrabi amesema ukandamizaji unaofanywa na vikosi vya ulinzi vya ndani vya taifa hilo umeendelea kuwa mkubwa, na hakuna uwajibikaji wowote kufuatia matatizo hayo.

Tuhuma kwa rais al-Sisi

Kwa ujumla ripoti yenyewe inamtuhumu rais Abdel Fattah al-Sisi kwa kuongoza nchi kimabavu na kwa ukandamizaji tangu kumuondoa madarakani mtangulizi wake, rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohammed Morsi mwaka 2013.

Rais wa Misri Abdel Fattah al-SisiPicha: picture-alliance/dpa

Amnesty, imesema mataifa 12 kati ya mataifa 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya yasalia kuwa wasambazaji wakubwa wa silaha na vifaa vingine vya matumizi kwa ajili ya polisi. Shirika hilo vilevile limesema hatua hiyo inakiuka makubaliono ya kusitisha kuipa silaha Misri ya umoja huo ambayo yaliridhiwa muda mfupi baada ya mauwaji ya mamia ya waanamanaji katika kile kilichoonekana kama matumizi makubwa kabisa ya nguvu kwa waandamanaji katika matukio ya Agosti 2013 nchini Misri.

Amnesty yenye makao yake makuu mjini London, Uingereza inasema hatua hiyo inaweza kufutiliwa mbali pamoja na kutokuwa na ufanisi.

Uidhinishwaji wa leseni za vifaa vya kijeshi

Kwa mwaka 2014 pekee, mataifa ya Umoja wa Ulaya yameidhinisha leseni 290 za vifaa vya kijeshi kwa Misri, vyenye gharama ya zaidi ya euro bilioni sita. Vifaa ambavyo mataifa hayo yaliviwasilisha kwa usafiri wa meli nchini humo ni pamoja na silaha ndogo ndogo, risasi, magari ya silaha, helkopta za kijeshi, silaha nzito na teknolojia ya ulinzi.

Pamoja na Marekani mataifa ya Ulaya yanayotajwa katika ripoti ambayo makampuni yake yanaingiza vifaa vya ulinzi ni pamoja nchini Misri ni pamoja na Uingereza, Ujerumani na Italia. Aidha taarifa hiyo imeyataja mataifa mengine kama Bulgaria, Cyprus, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, Hungary, Poland, Romania, Slovakia na Uhispania.

Brian Wood, mkuu wa udhibiti wa silaha na haki za binaadamu wa Amnesty amesema Umoja wa Ulaya unapaswa kusimamisha mara moja usafirishaji wake aina zozote za silaha na vifaa ambavyo vinatumiwa na Misri kufanya ukiukwaji wa haki za binaadamu.

Hata hivyo kufuatia lawama hizo mataifa ya Umoja wa Ulaya na Marekani yamesema yataendelea na bisahara yao ya silaha kwa Misri kwa kuwa ni mshirika wao madhubuti katika kanda hiyo tete.

Mwandishi: Sudi Mnette APE/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi