1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Urusi imefanya uhalifu wa kivita, Ukraine

6 Mei 2022

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International limesema leo kwamba kuna uthibitisho wa kutosha kwamba wanajeshi wa Urusi walifanya vitendo vya uhalifu wa kivita nchini Ukraine.

Amnesty International Protest Symbolbild
Picha: Alain Pitton/NurPhoto/picture alliance

Kulingana na shirika la kimataifa la Amnesty International visa walivyovirekodi ni pamoja na mauaji ya kiholela ya raia, mateso na kuyashambulia kwa mabomu makazi ya raia. Kulingana na shirika hilo, walifanya uhalifu huo walipokuwa wanashikilia maeneo yaliyo nje ya mji mkuu wa Ukraine, Kyiv. 

Taarifa ya kiuchunguzi ya shirika hilo iliyopewa jina "Harudi Tena" : Uhalifu wa kivita katika eneo la Kaskazinimagharibi mwa Kyiev, Oblast, imejikita katika mahojiano na tathmini ya kina ya ushahidi.

Katibu mkuu wa shirika la Amnesty International Agnès Callamard amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari mapema leo kwamba shirika hilo limerekodi mashambulizi yasiyo halali ya anga katika mji wa Borodyanka, na mauaji ya kiholela katika miji mingine na vijiji, ambavyo ni pamoja na Bucha, Andriivka na Vorzel.

Amesema kufuatia vitendo hivyo, Urusi haina budi kukabiliwa na mkono wa sheria kutokana na msururu huo wa makosa ya uhalifu yaliyofanywa kwenye eneo hilo.

"Tunajua kwamba uhalifu uliotendwa dhidi ya watu walio karibu na Kyiv ambao tunauripoti leo sio hadithi tu na wala sio bahati mbaya. Tunajua wao ni sehemu tu ya muundo unaodhihirsha mwenendo wa Urusi wa vitendo vya uhasama tangu mwanzo, muundo unaojirudia, wa kiwango cha juu na athari ya kutisha." alisema Callamard.

Katibu mkuu wa Amnesty International Agnes Callamard (katikati) akizungumza na wenzake walipokuwa wakitembelea maeneo mbalimbali Ukraine hivi karibuni.Picha: Eduardo Quiros Riesgo

Kulingana na shirika hilo, raia wa maeneo hayo walikabiliwa na unyanyasaji kama kufyatuliwa risasi kizembe na mateso wakati wanajeshi wa Urusi hao walipoanzisha mashambulizi nchini Ukraine, Februari 24.

Urusi ambayo inauita uvamizi wake nchini Ukraine "operesheni maalumu" ya kuipokonya silaha Ukraine na kuilinda dhidi ya mafashisti inakana wanajeshi wake kufanya uhalifu huo. Ukraine imesema inachunguza zaidi ya visa 9,000 vinavyohisiwa kuwa ni uhalifu wa kivita. Mahakama ya kimataifa ya makosa ya uhalifu, ICC pia inachunguza madai ya uhalifu huo wa kivita.

Ripoti hii ya Amnesty ni ya karibuni inayoelezea kunakili visa 22 vya uhalifu wa kivita uliofanywa na wanajeshi wa Urusi walipoyadhibiti maeneo ya Ukraine, kaskazinimagharibi mwa Kyiv ikiwa ni pamoja na mji wa Bucha ambako mamlaka zinasema zaidi ya raia 400 waliuawa.

Ujumbe wa Amnesty ulioongozwa na katibu mkuu huyo katika siku za karibuni umekuwa ukizuru eneo hilo na kuzungumza na manusura na familia za wahanga pamoja na kufanya mikutano na maafisa wa ngazi za juu za Ukraine.

Mashirika:RTRE/APE

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW