1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Uturuki yarejesha maelfu ya wahamiaji Syria

Yusra Buwayhid1 Aprili 2016

Shirika la Amnesty International linaituhumu Uturuki kurejesha mamia ya wahamiaji nchini Syria kila siku kinyume na sheria, huku wasiwasi ukizidi juu ya makubaliano ya kupokea wahamiaji kutoka Ugiriki

Bildergalerie Flüchtlingskinder Situation in Griechenland
Picha: DW/R. Shirmohammadi

Shirika hilo la kutetea haki za binaadamu la Amnesty limesema utafiti wake uliohusisha ukaguzi wa mpaka wa Syria na Uturuki unaonesha takriban Wasyria 100 wanarejeshwa kila siku nchini mwao ambako vita bado vinaendelea. Kwa maana hiyo maelfu ya wahamiaji wamesharejeshwa nchini Syria katika miezi ya hivi karibuni.

Hili linaleta wasiwasi kwa wahamiaji ambao watarejeshwa Uturuki kutoka Ulaya, chini ya mpango utakaoanza kutumika rasmi wiki ijayo, limesema shirika hilo.

Uturuki ilikubaliana na Umoja wa Ulaya mwezi uliopita, kuwapokea wahamiaji wote na wakimbizi waliovuka Bahari ya Mediterenia kinyume na sheria na kuingia nchini Ugiriki.

Na badala yake, nchi hiyo itapatiwa msaada wa kifedha, uwezekano wa Waturuki kusafiri bila ya visa barani Ulaya, pamoja na kuanzishwa tena mazungumzo ya Uturuki kujiunga na Umoja wa Ulaya. Lakini ripoti ya shirika la Amnesty inasema Uturuki sio nchi salama kwa wakimbizi huku ikiutilia wasiwasi uhalali wa mpango huwo.

Ripoti hiyo imesema maelfu ya wahamiaji wa Kisyria wamekuwa wakirejeshwa nchini mwao katika wiki saba hadi tisa zilizopita, hatua inayopingana na sheria za Uturuki, Umoja wa Ulaya pamoja na za kimataifa.

"Wakiwa wanalinda mipaka yao, viongozi wa Ulaya wamedharau jambo moja muhumi: kwamba Uturuki sio nchi salama ya kupokea wahamiaji wa Kisyria wanaokimbia vita, na inazidi kukosa usalama kila kukicha," amesema Mkurugenzi wa shirika hilo kwa upande wa bara la Ulaya na Asia ya Kati, John Dalhisen

Uturuki yapinga madai ya Amnesty

Kurugenzi wa shirika la Amnesty Internationa, kwa bara la Ulaya na Asia ya Kati John DalhuisenPicha: Amnesty International/Jon Hall

Kwa upande wake wizara ya mambo ya nje ya Uturuki imepinga madai hayo ya kwamba wahamiaji wa Kisyria wanarejeshwa nchini mwao kinyume na matakwa yao. Na kusema Uturuki imekuwa na sera ya kufungua "milango yake wazi" kwa wahamiaji wa Syria kwa miaka mitano na imekuwa ikizingazia kanuni ya kimataifa inayozuia kumjeresha mtu katika nchi ambayo atakabiliwa na mateso.

Maafisa wa wizara hiyo wameliambia shirika la habari la Reuters, miongoni mwa wahamiaji wa Kisyria walioomba hifadhi Uturuki, hamna aliyerejeshwa Syria kwa nguvu.

Aidha utafiti huwo uliofanywa na Amnesty unaonesha wengi wanaorejeshwa Syria, ni wale wahamiaji ambao hawakusajiliwa. Halikadhalika katika majimbo yaliyo kusini mwa Uturuki, uandikishaji wa wahamiaji unaonekana ukizoroto. Na wale wasiokuwa na vibali vya usajili, wananyimwa huduma za msingi kama vile huduma za afya na elimu.

Chini ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya pande hizo mbili, Uturuki inatakiwa kuwapokewa wahamiaji wanaorejeshwa kutoka Ugiriki kuanzia tarehe 4 mwezi huu. Lakini kuna wasiwasi juu ya idadi ya wahamiaji hao watakaorejeshwa, vipi watahudumiwa na kama watapatiwa mkaazi ya kutosha.

Lengo la mpango huwo ni kuifunga njia kuu ya kuingilia barani Ulaya ambayo ni bahari ya Aegean inayowaingiza wahamiaji hao Ugiriki, kwa matarajio ya kuendeela na safari hadi kaskazini mwa Ulaya katika nchi kama Ujerumani na Sweden.

Lakini shirika la Amnesty Internationa linasema namna Uturuki inavyorejesha maelfu ya wahamiaji nchini Syria, ni ishara kwamba mpango wa baina ya Umoja wa Ulaya na Uturuki una dosari. Ni mpango unaohitaji roho ngumu kutekelezwa, na usiotilia maanani sheria za kimataifa, limesema shirika hilo.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ape

Mhariri:Iddi Ssessanga

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW