1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Uungaji mkono wa Mahakama ya Afrika uongezwe

17 Julai 2026

Shirika la Amnesty International lataka nchi za Umoja wa Afrika kuongeza uungaji mkono wa kisiasa, kisheria na kifedha kwa Mahakama ya Afrika.

Mahakama ya Afrika-  Arusha  Tanzania
Jengo la Mahakama ya Afrika- Arusha Tanzania. Picha: Veronica Natalis/DW

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Watu (AfCHPR) inaadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake huku mashirika ya kutetea haki za binadamu yakitoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kuongeza uungaji mkono wa kisiasa, kisheria na kifedha kwa mahakama hiyo.

Katika ripoti mpya iliyotolewa kuadhimisha miaka 20 ya Mahakama hiyo, Shirika la Amnesty International limesema AfCHPR imekuwa chombo muhimu cha kuwapatia haki watu binafsi na mashirika ya kiraia ambao wameshindwa kupata suluhisho la ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi zao.

Maadhimisho hayo yanaangazia haja ya kulinda nafasi ya kiraia inayozidi kudorora barani Afrika na kuhakikisha nchi wanachama zinazingatia na kutekeleza maamuzi yanayotolewa na mahakama hiyo.

Hata hivyo, shirika hilo linaeleza kuwa bado kuna changamoto kubwa zinazokabili mahakama hiyo. Kati ya nchi 55 wanachama wa Umoja wa Afrika, ni nchi 34 pekee zilizoridhia itifaki ya kuanzishwa kwa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu na kufikia Julai 2026, ni nchi saba pekee zinazoruhusu watu binafsi na mashirika ya kiraia kuwasilisha malalamiko moja kwa moja. Baadhi ya nchi—ikiwemo Benin, Côte d'Ivoire, Rwanda, Tanzania na Tunisia—zimeondoa tamko hilo, na hivyo kuwanyima wananchi wao njia muhimu ya kutafuta haki.

Naibu Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini wa Amnesty International, Japhet Biegon, amesema Mahakama ya Afrika imeonyesha uwezo mkubwa katika kuchunguza kesi za ukiukwaji wa haki za binadamu, kutoa maamuzi muhimu na kupanua ulinzi wa haki hizo barani Afrika.

Mafanikio katika mizani ya haki

Tangu kuanza kazi rasmi mwaka 2006, Mahakama hiyo imehitimisha zaidi ya kesi 250, huku karibu kesi 150 zikiwa zimehusisha maamuzi kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu.

Amnesty International inaonya kuwa ufikiaji mdogo wa mahakama ya Afrika umeathiri uwakilishi wa baadhi ya maeneo ya Afrika.Picha: fikmik/YAY Images/IMAGO

Kesi hizo zimemulika masuala kama haki ya kusikilizwa kwa haki, heshima ya utu wa binadamu, kupinga mateso na ukatili dhidi ya wafungwa, pamoja na masuala yanayohusiana na uchaguzi.

Baadhi ya maamuzi muhimu ya Mahakama hiyo ni pamoja na hukumu dhidi ya Burkina Faso mwaka 2014 iliyosaidia kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari na kupambana na ukwepaji wa adhabu kwa wanaoshambulia waandishi wa habari. Pia, mwaka 2017, Mahakama hiyo ilitoa uamuzi uliotambua haki za jamii ya asili ya Ogiek nchini Kenya, huku mwaka 2023 ikitoa hukumu kuhusu athari za utupaji wa taka za kemikali kutoka meli ya Probo Koala nchini Côte d'Ivoire, ikisisitiza umuhimu wa kulinda mazingira na haki ya afya ya wananchi.

Pamoja na mafanikio hayo, Amnesty International inaonya kuwa ufikiaji mdogo wa mahakama hiyo umeathiri uwakilishi wa baadhi ya maeneo ya Afrika, hususan Afrika ya Kati, Kaskazini na Kusini mwa bara hilo.

Ripoti mpya ya Amnesty International pia inaonyesha utekelezaji hafifu wa maamuzi ya Mahakama ya Afrika, likitaka nchi zilizowahi kuhukumiwa kuhakikisha zinatekeleza kikamilifu maagizo yaliyotolewa. Aidha Baraza la Utendaji la Umoja Afrika limelaumiwa kwa kutokuwa makini katika kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ambayo ni lazima kufuatwa.

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu yenye makao yake makuu jijini Arusha, Tanzania, ina majaji 11 waliochaguliwa na Umoja wa Afrika. Ilianza rasmi shughuli zake Julai 2 mwaka 2006, ikiwa na jukumu la kulinda, kukuza na kutetea haki za binadamu kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.

https://www.amnesty.org/en/documents/ior60/1132/2026/en/

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW