1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Wahamiaji wapitia unyanyasaji mbaya Libya

15 Julai 2021

Ripoti ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International imesema wahamiaji wanaoshikiliwa katika kambi za mahabusu za Libya wanapitia unyanyasaji mbaya wa kingono mikoni mwa walinzi.

Griechenland Inoffizielles Flüchtlingslager in Samos
Picha: AFP/A. Messinis

Wahamiaji hao pia wanalazimishwa kutoa rushwa ya ngono ili kupata maji safi, chakula na mazingira safi. 

Ripoti hiyo, iliyojikita kwa wahamiaji waliokamatwa katika eneo la Mediterrenia na kupelekwa Libya mnamo 2020 na 2021, inaonyesha hali inazidi kuwa mbaya katika kambi licha ya hivi karibuni kambi hizo kuwekwa chini ya udhibiti wa wizara ya mambo ya ndani ya Libya. Soma UN: Vifo ya wahamiaji wanaovuka bahari kuelekea bara Ulaya vyaongezeka maradufu

Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki Papa Francis na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wametoa mwito wa kufungwa kwa kambi hizo.

Rushwa ya ngono 

Picha: Reuters/C. Baltas

Mwanamke mmoja anayeishi katika kambi hizo ameambia Amnesty International kuwa walinzi ndani ya  kambi huwabaka au kuwalazimisha wanawake kushiriki ngono kwa kubadilishana nao kuwa huru ama kupewa maji safi.

Ugunduzi huu unatokana na mahojiano na wakimbizi 53 na wahamiaji, wenye umri kati ya miaka 14 na 50, kutoka nchi kama Nigeria, Somalia na Syria, ambao wengi wao bado wako nchini Libya lakini waliweza kutoroka kambini au waliopata nafasi ya kutumia simu.

Baadhi ya wanawake wajawazito ndani ya kambi hizo waliiambia Amnesty Internationa kuwa wamekuwa wakibakwa mara kwa mara na walinzi, huku wanaume nao wakisema walilazimishwa kuvaa nguo za ndani pekee katika jaribio la kuwadhalilisha. Wengine, wakiwemo wavulana, walielezea kupapaswa, kuchochewa na kudhalilishwa.

Utendewaji huu usiyo wa kiutu unafuatia ripoti nyingi zilizowasilishwa tangu 2017 za watu kupigwa, kuteswa, ukosefu wa usafi wa mazingira na chakula.

Usalama wa wahamiaji

Picha: Getty Images/AFP/A. Pazianou

Amnesty International imesema walinzi wa pwani ya Libya wanaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya  wamewakamata baharini na kuwarudisha Libya watu 15,000 katika miezi sita ya kwanza mwaka huu, hii  ikiwa zaidi ya idadi jumla iliyorekodiwa mwaka 2020. Umoja wa Mataifa wasema wakimbizi wameongezeka maradufu katika muongo mmoja

Wakati data hizi haziaminiki, Amnesty imesema watu wengine 6,100 wamehamishiwa kambini mwishoni mwa  mwezi Juni.

Licha ya makubaliano kati ya pande zinazopigana za Libya tangu Oktoba kama sehemu ya mpango wa amani unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa kufuatia kupinduliwa kwa Muammar Gaddafi mnamo 2011, vikundi vyenye silaha bado vinaushawishi mkubwa na baadhi yao wanadhibiti kambi kadhaa za wahamiaji.

Baadhi ya wabunge wa Umoja wa Ulaya wameitaka Tume ya Ulaya pamoja na Halmashauri kuu ya Umoja huo, kuacha kufadhili walinzi wa pwani, wakisema kuwa Libya sio "nchi salama" kwa wahamiaji.

 

Reuters