1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: Watoto na vijana ni wahanga wa maandamano ya Iran

Sylvia Mwehozi
16 Machi 2023

Ripoti mpya ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International inasema kuwa watoto na vijana ni miongoni mwa raia wengi walioteswa na vikosi vya usalama dhidi ya maandamano ya kuipinga serikali.

Iran Teheran | Feiern zum 44. Jahrestag der Islamischen Revolution
Picha: AFP

Ripoti ya Amnesty International iliyotolewa siku ya Alhamisi, imeeleza kwamba waandamanaji wamekuwa wakipigwa, kuchapwa viboko na kupigwa shoti za umeme, kubakwa na kufanyiwa aina nyingine ya ukatili wa kijinsia kutoka kwa maafisa wa usalama tangu maandamano yalipoanza miezi sita iliyopita.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa mamlaka zilitumia ukatili dhidi ya vijana katika kuwazuia kuandamana. Mtaalamu kuhusu Iran katika shirika hilo nchini Ujerumani Dieter Karg amesema kwamba "ni jambo la kuchukiza kwamba viongozi wa umma wanatumia madaraka yao vibaya kwa njia hii kwa watoto walio katika mazingira magumu na wenye kuogopa na kuwasababishia maumivu makali na wasiwasi wao na familia zao na kuwaacha na makovu makali ya mwili na kiakili."Iran yamnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano

Aidha afisa huyo ameongeza kwamba "kwa kuwa hakuna matarajio ya kufanyika uchunguzi thabiti usio na upendeleo wa kuteswa kwa watoto nchini Iran" wanatoa wito kwa mataifa yote, ikiwemo serikali ya Ujerumani, kutumia mamlaka ya ulimwengu kwa maafisa wa Iran.

Kwenye ripoti hiyo, Amnesty International imeorodhesha ukatili dhidi ya watoto na vijana baada ya kukamatwa kwao, wakianza na vichapo katika magari ya kuwapeleka jela.

Huko gerezani, watoto walipigwa shoti za umeme kwenye maeneo yao ya siri, kulazimishwa kunywa dawa zisizojulikana na vipigo vikali, kwa mujibu wa ripoti. Ripoti inaongeza kwamba watoto, kama watu wazima walipelekwa kwa mara ya kwanza mara nyingi wakiwa wamefunikwa macho, hadi kwenye vituo vya mahabusu na kuhamishiwa kwenye magereza yanayotambulika baada ya wiki kadhaa za kuzuiliwa bila mawasiliano.

Maandamano pia yalifanyika katika miji ya UlayaPicha: Cédric Joubert/MAXPPP/picture alliance

Katika kisa kimoja, mama mmoja alisema maafisa wa serikali walimbaka mwanae wa kiume kwa kutumia bomba, huku wakimuweka katika kizuizi cha siri. Kabla ya kuwaachia huru watoto, maafisa wanasemekana kwamba waliwatishia wangewakamata jamaa zao ikiwa watalalamika kwa mtu yeyote kuhusu waliyopitia. Baadhi ya watoto waliopitia ukatili huo walikuwa wadogo wenye umri wa miaka 12. Ripoti ya shirika hilo imezingatia ushahidi wa watu waliokamatwa na ndugu zao.

Iran imekabiliwa na miezi kadhaa ya ghasia, zilizochangiwa na wimbi la maandamano ya kifo cha msichana wa Kikurdi, Mahsa Amini. Msichana huyo alifariki dunia akiwa mikononi mwa polisi mwezi Septemba, mwaka uliopita siku chache baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka kanuni za mavazi ya Kiislamu.

Tangu wakati huo vijana wameshiriki katika maandamano dhidi ya mwenendo wa ukandamizaji wa serikali na mfumo wa kiutawala wa Kiislamu wa Tehran. Shirika la Amnesty International linaamini kwamba vijana wengi walikuwa na chini ya umri wa miaka 25 na huenda maelfu ya watoto walikamatwa. Siku chache zilizopita, mahakama nchini humo ilibainisha kwamba kiasi ya waandamanaji 22,000 walikamatwa katika miezi iliyopita. Wengi wao wanasemekana kuwa wameachiwa huru ingawa hakuna takwimu rasmi.Iran yashutumiwa kimataifa kwa kumnyonga muandamanaji

Naibu mkurugenzi wa Amnesty International katika eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini Diana Eltahawy, alisema kuwa "maafisa wa serikali ya Iran wamewanyakua watoto kutoka kwenye familia zao na kuwafanyia ukatili usioeleweka."

Shirika hilo limetoa wito wa kuachiliwa huru kwa watoto hao wadogo waliozuiliwa na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha maafisa wa Iran kwa ghasia hizo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW