1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yailaumu Urusi kwa mashambulizi Syria

Yusra Buwayhid23 Desemba 2015

Shirika la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International linaishutumu Urusi kulenga raia katika mashambulizi yake Syria. Naye baba wa mtoto wa Kisyria Aylan Kurdi, ameitolea wito dunia kupokea wakimbizi wa Syria.

Syrien Russische Luftangriffe
Picha: picture-alliance/AA/M. Khder

Watetezi wa haki za binaadamu wa shirika la Amnesty International wanaishutumu Urusi kuwa inatumia mabomu ya mtawanyiko katika maeneo ya raia nchini Syria na mashambulizi hayo yanasemekana tayari yameshasababisha vifo vya mamia ya watu katika miezi michache iliyopita.

Ripoti iliyotolewa na shirika hilo inasema kwamba kumekuwa na taarifa kadhaa juu ya kudodonshwa kwa mabomu hayo ya mtawanyiko na vikosi vya Urusi na yanayolenga maeneo ya raia tangu nchi hiyo ilipojitumbukiza katika mgogoro wa Syria Septemba 30 mwaka huu.

Hata hivyo maafisa wa Urusi wamekuwa wakikanusha shutuma hizo, na wakaazi pamoja na wanaharakati wa upande wa upinzani nchini Syria wanakubali kuwa hawana njia ya kuwa na uhakika ni nani baina ya Urusi na vikosi vya serikali wanaodondosha mabomu hayo.

"Nataka kuweka wazi kwamba kila tukijaribu kufanya mashambulizi kwa uangalifu zaidi, ndipo mashirika ya kutetea haki za binaadamu yenye makaazi yake mjini London yanapoendelea kutushutumu kulenga raia, lakini mpaka sasa hawakuweza kuthibitisha maneno yao kwa ushaidi kamili," amesema Jenerali Igor Konachenkov wa wizara ya Ulinzi ya Urusi.

Mabomu ya aina hii kawaida huzama chini ya ardhi na kuripuka bila ya kutarajiwa katika siku za mbele. Hili linaweza kuhatarisha maisha ya raia hata baada ya mapigano kumalizika katika miaka ya baadae.

Baba wa Aylan Kurdi aitolea wito dunia

Abdullah Kurdi baba wa mtoto Aylan KurdiPicha: Reuters/G. Gurbuz

Aidha baba wa mtoto wa Kisyria Aylan Kurdi ambaye maiti yake ilikutikana katika ufukwe wa Uturuki miezi michache iliyopita na kuzua mjadala mkubwa kuhusu mgororo wa wakimbizi wa Syria, ametoa wito wa Krismasi kwa dunia nzima kuiomba kufungua milango yake kwa wakimbizi wa mzozo wa Syria.

Ujumbe wake unaotarajiwa kurushwa na kituo cha televisheni cha Uingereza cha channel 4 siku ya Krismasi, unakuja baada ya shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa kusema kwamba zaidi ya wahamiaji na wakimbizi milioni moja wamewasili barani Ulaya ndani ya mwaka huu pekee. Miongoni mwa hao ni wale 970,000 waliofanya safari ya hatari ya kuvuka bahari ya Mediterenia.

Aylan aliyekuwa na umri wa miaka mitatu alifariki dunia mwezi Septemba baada ya familia yake, iliyokuwa ikijihifadhi nchini Uturuki ikikimbia vita vya Syria, kuamua nayo kufanya safari ya aina hiyo kwa kutumia boti ndogo isiyo na usalama kwa lengo la kujaribu kukimbilia nchini Ugiriki.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/ape/rtre

Mhariri:Iddi Ssessanga