Amnesty yakosoa unyanyasaji wa wahamiaji nchini Tunisia
6 Novemba 2025
Kwenye ripoti yake mpya iliyotokana na utafiti wa kati ya Februari 2023 na Juni 2025, Shirika la Amnesty ambalo liliwahoji wakimbizi na wahamiaji karibu 120, wengi wao kutoka Guinea, Sudan na Sierra Leone, limesema mfumo wa sasa wa kuomba hifadhi na uhamiaji wa nchini Tunisia una viashiria vya kibaguzi na ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu.
Limesema mfumo huo hauzingatii hata kidogo haki ya kuishi, usalama na utu wa wakimbizi na wahamiaji na hasa "weusi." Kulingana na shirika hilo, wachunguzi wake wamekusanya ushuhuda wa kutisha unaohusiana na uhalifu usio wa kibinaadamu wa ngono, vipigo vikali pamoja na mateso mengine makali dhidi ya wahamiaji. Kikosi cha Ulinzi wa Taifa ndicho kinachotuhumiwa kufanya uhalifu huo.
Serikali ya Tunis yajitetea
Lakini jana Jumatano, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tunisia Mohamed Ali Nafti alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema wahamiaji wote walioingia kwenye eneo la Tunisia kinyume cha utaratibu watarejeshwa kwa kuzingatia misingi ya kiutu.
Tunisia imekuwa ikitumika kama kituo cha kuanzia safari za hatar na wahamiaji ambao wengi wao wanatokea kusini mwa Jangwa la Sahara, wanaojaribu kuvuka Bahari ya Mediterania kila mwaka wakikimbilia Ulaya kusaka maisha bora.
Sera ya taifa hilo la Afrika Kaskazini kuhusu uhamiaji usio wa kawaida ilibadilika mwaka wa 2023. Na kulingana na Amnesty maafisa wa ngazi za juu kabisa wa Tunisia walikuwa ni miongoni mwa waliochochea chuki za kikabila na chuki dhidi ya wageni.
Hotuba ya Rais Saied ilichochea ubaguzi
Mwezi Februari mwaka huo, Rais Kais Saied wa Tunisia alinukuliwa akisema "makundi ya wahamiaji haramu" yalikuwa yakitishia kuvuruga muundo wa idadi ya watu katika nchi hiyo yenye Waarabu wengi.
Hotuba hiyo ilisababisha kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya watu weusi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa ripoti ya Amnesty, ambapo "vikundi vya watu vilishawambulia wakimbizi na wahamiaji weusi mitaani", lakini pia likiwashutumu walinzi wa pwani mwa Tunisia kufanya vitendo vilivyohatarisha maisha ya watu na hata kusababisha vifo.
Wakimbizi 14 pamoja na wahamiaji waliiambia Amnesty kwamba walibakwa ama kushuhudia wenzao wakibakwa, lakini pia walifanyiwa vitendo vingine vya unyanyasaji wa kingono na mamlaka za usalama za Tunisia.
Kundi hilo pia limeukosoa Umoja wa Ulaya kwa kuingia makubaliano na Tunisia ya kukabiliana na uhamiaji usio wa kawaida likisema hatua hiyo iichukuliwa katikati ya ongezeko kubwa la matukio ya ubaguzi wa rangi na wala hayakuzingatia kulinda haki za kiutu.