1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yashutumu mauaji ya raia mzozo wa Msumbiji

2 Machi 2021

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International limezilaumu pande tofauti katika mzozo wa jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji - jeshi la serikali, mamluki na wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab kwa mauaji ya raia.

Ankommen in Metuge, Hilfe für Mosambik
Picha: Estácio Valói

Katika ripoti yake mpya iliyotolewa Jumatatu jioni mbele ya waandishi habari kwa njia ya vidio mjini Berlin, Shirika hilo la kimataifa la utetezi wa haki za binadamu limezinyooshea kidole pande zinazohusika katika mzozo wa jimbo la Cabo Delgado kwa mauaji ya mamia ya raia wasio na hatia.

Ripoti hiyo ina kichwa cha maneno kinachosema,''Nilichokiona ni kifo: Uhalifu wa kivita katika jimbo lililosahaulika la Cabo Delgado.

Soma pia: Ureno kuisadia Msumbiji kupambana na waasi

Inaelezwa kwamba haki za binadamu zimekiukwa kwa kiwango kikubwa katika mgogoro unaoshuhudiwa kwenye jimbo hilo la Kaskazini mwa Msumbiji ambapo yanahusika makundi yenye silaha ya ndani ya nchi hiyo.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeandika ripoti hii baada ya kuzungumza na watu 79 kutoka jamii 15 kwenye eneo hilo.

Katika jimbo hilo mauaji makubwa yamefanyika na uharibifu kwa wakati mmoja na umma wa eneo hilo umejikuta umenasa katikati baina ya vikosi vya usalama vya Msumbiji, wanajeshi mamluki kutoka kampuni ya kibinafsi ya kijeshi ya Afrika Kusini, DAG na kundi la wanamgambo wenye silaha wa itikadi kali, la Al-Shabaab.

Soma pia: Watu 40 wafa maji wakikimbia machafuko Msumbiji

Ulrich Fehling mtaalamu kuhusu Msumbiji, kutoka Amnesty International, tawi la Ujerumani anasema makundi yote hayo matatu yamehusika kuvunja haki za binadamu katika machafuko hayo na yana dhamana ya mauaji ya mamia ya watu.

Wanachama wa kundi la itikadi kali la Al-Shabab, la Msumbiji walilenga mashambulio yao dhidi ya raia, na kuvitia moto vijiji pamoja na miji huko kaskazini mwa nchi hiyo na kufanya vitendo vingine vingi vya mauaji katika mashambulizi hayo.

Watoto waliokimbia miji yao ya nyumbani kwa sababu ya ugaidi mkoani Cabo Delgado. Picha: Roberto Paquete/DW

Mauaji ya Quissanga

Mojawapo ya matukio yaliyoripotiwa kuhusu machafuko ya kaskazini mwa Msumbiji ni uvamizi uliofanywa na kundi hilo la Alshabab mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2020 katika mji wa Quissanga na kuwateka nyara vijana kadhaa baada ya kushambulia.

Wengi wa wasichana na wanawake walioachwa bila makaazi walikimbia hujuma za wanamgambo hao wakihofia kutekwa nyara, kubakwa au kuozwa kwa lazima.

Soma: Msumbiji: Ugaidi waongezeka katika jimbo la Cabo Delgado

Lakini pia ripoti ya Amnesty International inasema kwamba katika harakati za kuwaandama wapiganaji wanaodaiwa kuwa wa kundi la Al-Shabab, jeshi la nchi hiyo na askari polisi pia waliendesha matukio ya kuuwa watu kinyume cha sheria, kuwatesa au kuwanyanyasa pamoja na kukatakata viungo vya miili ya waliouwa.

Wanajeshi wa Msumbiji waliwakamata watu wa jinsia ya kiume, kuwafunga nyuso zao kwa vitambaa na kuwapiga risasi wengi wao kabla ya kuifukia miili yao kwenye kaburi la pamoja. Imeelezwa kwamba wanawake walichukuliwa na kupelekwa katika kambi ya jeshi walikobakwa na vikosi vya usalama.

Vikosi vya usalama vya Msumbiji vinashutumiwa pia kwa kufanya mauaji ya raia jimboni Cabo Delgado.Picha: Roberto Paquete/DW

Mamluki wa serikali kutoka Afrika Kusini

Lakini pia baada ya vikosi vya usalama vya serikali ya Msumbiji kushindwa mara kadhaa na wapiganaji wa Al-Shabab katika mapambano, serikali ya nchi hiyo iliamua kukodisha mamluki kutoka kampuni ya kibinafsi ya kijeshi kutoka Afrika Kusini kwa kifupi ikiitwa DAG. Wanajeshi hao mamluki walitakiwa kuwasaidia wanajeshi wa serikali katika vita hiyo kupitia mashambulizi ya anga.

Mamluki hao walifyetua risasi pamoja na kurusha maguruneti bila ya kujali kutokea kwenye helikopta zao dhidi ya mikusanyiko ya watu. Waliendelea kushambulia majengo ya umma ikiwemo Hospitali, shule na makaazi ya watu.

Soma: Wapiganaji wa itikadi kali waua watu 52 Msumbiji

Ulrich Fehling afisa wa Amnesty International nchini Ujerumani anasema jumuiya ya kimataifa imeshindwa kutambua na kuchukua hatua juu ya mgogoro huu kwa wakati mwafaka, wakati serikali ya Msumbiji nayo ikionesha kutokuwa na nia ya kuwalinda wananchi wake.

Ongezeko la wakimbizi wa ndani Msumbiji

01:25

This browser does not support the video element.

Fehling anasema mgogoro huu sasa umeongezeka na kuwa vita kamili ya makundi yenye silaha ya Msumbiji, na jumuiya ya kimataifa inapaswa hivi sasa kufanya kazi kuhakikisha mashambulizi dhidi ya raia yanakomeshwa mara moja na wale waliohusika kwenye hujuma wafikishwe mbele ya sheria.

Chanzo: Amnesty International

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW