1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yataka vifo vya waandamanaji Kenya vichunguzwe

25 Septemba 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International, linapanga kuwasilisha ombi la kutaka kuundwe tume ya kuchunguza vifo vya watu kadhaa kutokana na matumizi ya nguvu ya polisi kinyume cha sheria.

Kenya-Naiirobi -Maandamano
Polisi akifyatua bomu la machozi kutawanya waandamanajiPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

Miezi mitatu baada ya maandamano makubwa ya kuipinga serikali nchini Kenya, Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International, leo linapanga kuwasilisha ombi la kutaka kuundwe tume ya kuchunguza vifo vya watu kadhaa kutokana na matumizi ya nguvu ya polisi kinyume cha sheria.

Kwa kuzingatia picha na mahojiano na mashuhuda, wanasheria na wataalamu wa matibabu, Amnesty imesema polisi ilitumia silaha hatari dhidi ya maandamano ya amani, na kuwaua takriban waandamanaji sita.

Irungu Houghton, mkuu wa shirika hilo la Amnesty nchini Kenya, amesema haki ya kuandamana nchini Kenya inalindwa chini ya katiba na kwamba haikubaliki kwamba badala ya kuwawezesha na kuwalinda waandamanaji, polisi iliamua kutumia nguvu dhidi yao.

Ombi hilo la Amnesty linaadhimisha miezi mitatu tangu siku hiyo iliyoghubikwa na matukio ya kushangaza wakati waandamanaji walipovamia jengo la bunge mjini Nairobi mnamo Juni 25.