Amnesty yataka vikwazo vya silaha kote Sudan
25 Julai 2024Shirika hilo limesema katika ripoti yake kuwa, vita nchini Sudan kati ya jeshi na kikosi cha wanamgambo cha RSF vinachochewa na usambazaji wa silaha usiozuiliwa na washirika kutoka sehemu nyengine duniani wanaounga mkono pande zinazohasimiana nchini humo.
Ripoti ya Amnesty International iliyopewa jina la "Silaha mpya zinachochea vita Sudan," imegundua hivi karibuni kuwa silaha kutoka mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Urusi, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Serbia, Yemen na China zimeingizwa Sudan ili kutumika katika uwanja wa mapambano.
Mkuu wa kitengo cha utafiti wa migogoro wa Amnesty International Brian Castner ameliambia shirika la habari la AFP kuwa maelfu ya silaha zinaingizwa Sudan na kuchochea ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.