Amnesty yawatuhumu Wanajeshi wa DRC kwa uhalifu
11 Desemba 2024Wanajeshi hao wanashutumiwa uhalifu huo kufuatia mauaji ya mwaka jana katika mji wa kaskazini mashariki wa Goma ambapo watu 56 waliuawa. Maafisa waliotajwa katika ripoti hiyo iliyotolewa siku ya Jumatano ni Constant Ndima Kongba, aliyekuwa gavana wa kijeshi wa jimbo la Kivu Kaskazini, maafisa wa jeshi Kanali Mike Mikombe Kalamba na Meja Peter Kabwe Ngandu.
Wanajeshi hao walivamia hekalu la kikundi cha kidini huko Goma mnamo Agosti 30, 2023 na wengi wa waathiriwa walikuwa wanachama wa kundi hilo la kidini ambalo kiongozi wake aliitisha maandamano ya kutaka mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali na kikosi cha Umoja wa Mataifa kuondoka katika eneo hilo.
Soma pia: Amnesty yaitaka Kongo ichukue hatua za kulinda haki za raia
Wakati huo, mamlaka zilisema watu 56 waliuawa, lakini ripoti ya siri ya Umoja wa Mataifa ambayo Amnesty ilipata nakala yake ilisema idadi ya vifo ilifikia watu 102, ikiwa ni pamoja na wanaume 90, wanawake wanane na wavulana wanne, huku wengine 80 wakijeruhiwa.