1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty yazilaum China, Ukraine, Sudan kwa kuuza silaha hovyo nchini S. Kusini

Admin.WagnerD29 Juni 2012

Shirika la haki za binadamu la Amnesty International, limezilaumu nchi za China, Ukraine na Sudan kwa kuchochea vifo vya raia wasio na hatia nchini Sudan Kusini, kwa kuyauzia silaha makundi yanayohasimiana nchini humo.

Kifaru cha kivita.
Kifaru cha kivita.Picha: Fotolia

Katika ripoti yake iliyowasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Amnesty ilisema Sudan Kusini inayojiandaa kusherehekea mwaka moja wa uhuru wake, inakabiliwa na migogoro kadhaa katika nyanja za kiusalama, kiuchumi na kibinadamu.

Sudan Kusini ilijitenga rasmi na utawala wa Khartoum Julai 9, 2011 na tangu wakati huo, nchi hiyo imekuwa katika migogogoro ya mara kwa mara na jirani huyo wa kaskazini, ikihusisha mafuta, na mkoa wa mpakani wa Abyei.

Sudan kusini imefunga visima vingi vya mafuta na hivyo kukosa karibu asilimia 98 ya mapato yatokanayo na bidhaa hizo, ilisema ripoti ya Umoja wa Mataifa na kuonya juu ya mgogoro wa kiuchumi unalikabili taifa hilo linaloteswa na umaskini mkubwa kwa raia wake.

Wanajeshi wa SPLA nao wamelaumiwa kwa kuua raia bila kuchagua.Picha: dapd

Marekani yaonya juu ukandamizaji
Nchini Marekani, msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Victoria Nuland alielezea wasiwasi wa nchi hiyo juu ya kamatakamata na kufungwa kwa raia wanaoandamana kupinga hali ngumu ya kiuchumi nchini Sudan Kusini.

Nuland alisema njia hii inayotumiwa naserikali ya Sudan Kusini kutatua matatizo siyo sahihi na kwamba inaonyesha serikali hii inaweka nguvu zake katika sehemu isiyo badala ya kuzielekeza katika kutatua matatizo yanayowakabili raia. Aliongeza kuwa serikali ya Juba inapaswa kumaliz tofauti zake na Sudan na kutekeleza vipengele vyote vya mkataba wa amani ili iweze kusonga mbele.

Amnesty ilisema mapigano yamesababisha ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu katika majimbo ya Mayom na Unity nchini humo na kwamba matumizi mabaya ya silaha yamesababisha vifo vya raia wengi na kuwalaazimisha maelfu kuyahama makaazi yao.

Ripoti hiyo iliyalaumu majeshi ya serikali ya Sudan Kusini - Sudan People's Liberation Army (SPLA) na kikundi cha upinzani cha South Sudan Liberation Army (SSLA) kwa kuwalenga raia wasio na hatia kati ya mwaka 2010 na 2011.

Wanajeshi wa SPLA nao wamelaumiwa kwa kuua raia bila kuchagua.Picha: dapd

SIlaha kutoka China, Sudan, Ukraine
Mkurugenzi wa Amnesty anayeshughulika na bara la Afrika, Erwin van der Borght, alisema serikali laazima ziache kuuza silaha nchini Sudan Kusini, ambazo zinatumiwa kufanya ukiukaji wa sheria za kimataifa kuhusu haki za binadamu, hadi pale nchi hiyo itakapoweka mifumo ya mafunzo na uwajibikaji inayoeleweka.

Amnesty ilisema silaha zinazouzwa nchini humo ni pamoja na mabomu ya ardhini ya kuripuria magari kutoka China, ambayo yalitegwa kwa wingi katika mkoa wa Unity, makombora kutoka sudan na vifaru vya kivita aina ya T-72 kutoka Ukraine. Shirika hilo lilisema Sudan kusini ilitumia vifaru hivyo kushambulia makaazi ya raia bila kuchagua.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, vifaru hivyo vilipelekwa Sudan Kusini kupitia nchi za Kenya na Uganda kwa msaada wa makampuni ya meli yaliyoko Ujerumani, Ukraine na kisiwa cha Uingereza cha Man. Pia Sudan kusini ilipata idadi kubwa ya silaha aina ya AK-47, bunduki za rasharasha nyepesi na nzito na mota.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\DPAE\AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW