Amri mbadala ya Donald Trump Magazetini
7 Machi 2017Tunaanzia Marekani ambako rais Donald Trump ametia saini amri mbadala inayowazuwia wakimbizi na wakaazi wa nchi sita, badala ya saba kuingia nchini humo . Gazeti la "Nürnberger Nachrichten" linaandika: "Na vizuwizi vya sasa pia vya kuwapokea wakimbizi vinatia wasi wasi. Hadi wakati huu kila aliyekuwa na kinga ya ukimbizi, aliyetaka kuhamia nchini humo, alibidi akabiliane na uchunguzi wa kina wa maafisa wa idara mbali mbali za Marekani kwa muda wa miaka miwili. Hakuna nchi yoyote nyengine yenye vizingiti vya juu kama hivyo duniani. Kwa kutia saini amri hii mbadala, Donald Trump anataka kujionesha yeye ndie mwenye kuamua, na yeye ndie mwenye kutekeleza ahadi alizotoa katika kampeni za uchaguzi."
Amri Mbadala pia inakosolewa
Gazeti la "Badische Zeitung" linahisi na amri hii mpya pia itapingwa mahakamani. Gazeti linaendelea kuandika: "Trump anajitafutia mwenyewe mashaka. Amesubiri zaidi ya wiki moja kutia saini amri mbadala na hayo pekee yanathibitisha kwamba hali si hatari hivyo. Watu wangeamini kwa urahisi zaidi hoja kwamba lengo lake halikushawishiwa kidini, kama katika kampeni zake za uchaguzi hakuwa akizungumzia kuwapiga marufuku waislam kuingia nchini humo. Nchi kadhaa husika, wakaazi wake wengi ni waislam : Amri ya kwanza iliweka wazi kabisa kwamba wakristo hawahusiki. Ni shida kwamba hali hiyo haitotiliwa maanani kesi nyengine zitakapofunguliwa. Na mashitaka hayatokosekana pia dhidi ya amri hii mpya."
Mvutano kati ya Ujerumani na Uturuki wazidi makali
Mada yetu ya pili magazetini inahusiana na mvutano unaoutikisa uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki. Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika: "Serikali kuu ya Ujerumani italazimika kutathmini upya uhusiano wake na Uturuki baada ya kura ya maoni ya kuifanyia mabadiliko katiba ya nchi hiyo. Pindi Erdogan akishinda, mfumo wa kisiasa wa Uturuki utabadilika moja kwa moja na kugeuka kuwa mfumo ambapo rais atakuwa na madaraka makubwa kupita kiasi. Mfumo kama huo unahitaji sheria za aina mpya na sio zile zinazotumika kukabiliana na wapenda demokrasia wanaoangaliwa kuwa ni washirika na marafiki. Na hata kama Erdogan atashindwa, wajerumani hawastahiki kuendelea na hali ya mambo kama zamani. Serikali kuu ya Ujerumani inabidi ijiandae kukabiliana na Uturuki ya aina nyengine, japo kama itaendelea kuwa mwanachama wa jumuia ya kujihami ya NATO, lakini itaaachana na maombi ya kujiunga na Umoja wa ulaya. Itaibuka Uturuki nyengine ambayo watu watabidi washirikiane nayo kwa masilahi ya kila upande-kwa mfano katika kuheshimu makubaliano kuhusu wakimbizi-ingawa na hapo pia patahitajika mipaka.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Yusuf Saumu