1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri mpya ya rais Trump yalenga mataifa yale yale

21 Februari 2017

Amri ya rais Donald Trump kuwapiga marufuku wasafiri ambayo amesema ataifanyia marekebisho bado inayalenga mataifa yale yale yaliyoorodheshwa kwenye ile amri yake ya awali iliyosimamishwa na mahakama.

USA Präsident Donald Trump
Rais Donald trumpPicha: picture-alliance/abaca/O. Olivier

Amri hiyo lakini haiwajumuishi wasafiri walio na Visa ya kuingia Marekani. Afisa wa ngazi ya juu katika uongozi wa Marekani, amesema amri hiyo ambayo Trump ameipitia upya itayalenga mataifa yale yale saba yenye idadi kubwa ya waislamu duniani, ambayo ni  Iraq, iran, Syria, Yemen, Somalia, Sudan na Libya.

Afisa huyo amesema kwamba wale walio na kibali cha kuingia Marekani yaani green card na hivyo kuwa na uraia wa nchi mbili, Marekani na mojawapo ya nchi hizo saba wataruhusiwa kuingia nchini humo. Rasimu hiyo mpya pia haiwaagizi tena maafisa kuwachagua wakimbizi kutoka Syria na kuwanyima visa wanapowasilisha maombi yao.

Afisa huyo alizungumzia ripoti hiyo kabla kutolewa kwake rasmi ingawa hakutaka atajwe jina. Amesema rasimu hiyo inaweza kubadilishwa kabla kutiwa sahihi, jambo ambalo Trump anasema litafanyika wiki hii.

Alipoulizwa kuhusiana na amri hiyo mpya, msemaji wa ikulu ya White House Sarah Huckabee Sanders alisema ile inayosambazwa kwa sasa ni rasimu tu na kwamba stakabadhi ya mwisho itatolewa karibuni. Idara ya usalama wa ndani haikutoa jawabu ilipoulizwa kuhusiana na kauli yake.

Amri ya kwanza ilizua mtafaruku

Amri ya kwanza ya rais iliyotolewa na Trump ilizua mtafaruku katika viwanja vya ndege kote duniani, kwa kuwa wasafiri walizuiwa mara tu amri hiyo ilipoanza kutekelezwa na walio na uraia wa kudumu nchini Marekani kupitia green card, walikuwa miongoni mwa hao waliozuiwa kuingia nchini humo.

Waandamanaji katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa San FranciscoPicha: Getty Images/Lam

Majaji walitoa usaidizi wa kisheria kwa wale waliozuiliwa na waliopinga waliandamana hadi kwenye viwanja vya ndege pindi tu habari za kutekelezwa kwa amri hiyo zilipoenea. Amri hiyo ya kwanza ilikuwa imewazuia raia wa nchi hizo saba kuingia Marekani katika kipindi cha siku 90.

Mwaka huu Marekani tayari imewakubalia wakimbizi 35,000 kuingia nchini humo, na nafasi zilizosalia kwa ile idadi anayoitaka Trump ya wakimbizi watakaoingia Marekani kutimia ni 15,000, haya ni kwa mujibu wa afisa wa Marekani. Hii ina maana kwamba kwa mda uliosalia wa mwaka huu wa kifedha, idadi ya wakimbizi wanaokubaliwa kuingia Marekani kila wiki itapungua mno ikilinganishwa na ile ya uongozi wa Barack Obama.

Trump anaifanyia marekebisho amri yake ya kwanza

Mapema mwezi huu mahakama ya rufaa huko San Francisco ilikataa kuirejesha marufuku ya Trump, na ikakataa pia madai ya uongozi wake kwamba ni amri ya rais, ikisema kuwa malengo yake hayakuwa mazuri. Hatua hiyo ilimfanya Trump kuweka ujumbe kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Twitter uliosema, "tuonane mahakamani", na tokea wakati huo ameishambulia mahakama hiyo akisema ilitoa uamuzi uliochochewa kisiasa.

Maelfu walijitokeza katika jiji la Denver, kupinga amri hiyoPicha: picture-alliance/AP Photo/B. Linsley

Waziri wa usalama wa ndani John Kelly alisema siku ya Jumamosi Trump anaifanyia marekebisho amri yake ya rais iliyozuia raia wa nchi saba kuingia Marekani, kuangalia matatizo yaliyoifanya ikataliwe na mahakama.

Alipozungumza katika ule mkutano wa usalama ulioandaliwa Munich, Ujerumani, Kelly alisema amri ya kwanza ya Trump ilikua ni ya kuhakikisha watu kutoka mataifa hayo wanasitishwa kuingia Marekani kwa muda ili kuangalia pale palipo na mapungufu kwenye mfumo wa uhamiaji wa Marekani na kufanya mageuzi.

Mwandishi: Jacob Safari/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman