ANC hatarini kushindwa katika miji mikubwa
5 Agosti 2016Chama cha Democratic Alliance - DA kimeshinda Port Elizabeth, mji wa viwanda ulioko pwani ya kusini, kwa karibu asilimia sita, na kujipatia ushindi katika eneo muhimu la uchaguzi wa manispaaa.
Wakati karibu kura zote zimekwishahesabiwa mjini Port Elizabeth, chama cha DA chenye asimilia 47 ya kura-- hakijashinda wingi wa moja kwa moja na kitahitaji kuunda muungano na vyama vidogovidogo.
"Tumeshinda Nelson Mandela Bay. Sijui kama tumepata wingi wa moja kwa moja, lakini bila shaka sisi ndiyo tutakuwa chama kikubwa zaidi, tutakuwa tunaunda serikali pamoja," alisema mgombea wake wa umeya katika manispaa ya Nelson Mandela Bay, Athol Trollip amesema.
Pigo kwa ANC
Katika mabadiliko ambayo hakikuyatarajia, chama cha ANC kilichoasisiwa na Nelson Mandela, kimepata pigo lake la kwanza kubwa katika manispaa inayojulikana kama Nelson Mandela Bay.
Likijumlisha mji wa Port Elizabeth na vijiji vya jirani, eneo hilo lilikuwa kiota cha harakati za kupinga ubaguzi wa rangi na utengano- Apartheid, na lilipata jina hilo mnamo mwaka 2001.
"Tunakubalia kuwa tumeshindwa Port Elizabeth," alisema Jackson Mthembu, mnadhimu mkuu wa ANC bungeni, kabla ya kutangazwa kwa matokeo ya mwisho katika miji iliyokuwa na ushindani mkali ya Johannesburg - ambao ndiyo mji wa kiuchumi, na mji mkuu wa Pretoria.
Mthembu alisema wanatambua kuwa uchaguzi huu ulikuwa na ushindani mkubwa lakini ana uhakika wataibuka na ushindi Pretoria na Johannesburg.
Matokeo mabaya zaidi tangu 1994
Huku karibu asilimia 90 ya kura zikiwa zimehesabiwa, ANC ilikuwa mbele katika matokeo jumla, lakini huu ndiyo uchaguzi ambamo kimefanya vibaya zaidi tangu kuanguka kwa utawala wa wepue wachache miaka 22 iliyopita.
Wakati zoezi la kuhesabu likikaribia kumalizika chama hicho cha Mandela kilikuwa na asilimia 54 --- hii ikiwa pungufu kabisaa kutoka asilimia 62 kiliyopata katika uchaguzi wa mwisho wa manispaa uliyofanyika mwaka 2011.
ANC kilikuwa kinashinda kwa zaidi ya asilimia 60 katika chaguzi zote tangu uchaguzi wa kwanza uliyowahusisha wapigakura wa rangi na tabaka zote mwaka 1994, wakati ambapo Mandela aliapishwa kuwa rais wa kwanza mwafrika.
Hukumu dhidi ya rais Zuma
Chama cha DA kilikuwa na asilimia 26 ya kura jumla, huku chama cha siasa kali za mrego wa kushoto - Economic freedom Fighters EFF, kikiw ana asilimia 8 kwa mujibu wa matokeo rasmi yaliyotolewa leo asubuhi.
Uchaguzi huo uliyofanyika siku ya Jumatano, ulikuwa unatazamwa na wengi kama hukumu kuhusu utendaji wa Rais Jacob Zuma, ambaye amekumbwa na mkururo wa kashfa tangu alipoingia madarakani mwaka 2009.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre.
Mhariri: Saumu Yusuf