Ofisi yake imeeleza kusikitishwa na uamuzi huo
13 Oktoba 2017Saa chache baada ya Mahakama ya Rufaa Afrika Kusini kutoa uamuzi kuwa Rais wa nchi hiyo Jacob Zuma hana budi kujibu mashtaka ya rushwa na ubadhirifu yanayomkabili, baadhi ya wanachama wa ANC wameshauri kiongozi huyo ajiuzulu ili kulinda heshima ya chama hicho.
Zuma anaendelea kuongoza katika muhula wake wa pili utakaomalizika 2019.
Hata hivyo, ofisi ya rais Zuma imeeleza kusikitishwa kwake na uamuzi huo na kusema kuwa wataendelea kupambana ili rais huyo asishtakiwe huku wakisisitiza kuwa wanatarajia uamuzi wa haki utafanywa.
Kadhalika chama kikuu cha upinzani , Democratic Alliance kimesisitiza kuwa kitamuandikia Mwendesha Mashtaka mkuu wa Serikali ili kuhimiza Rais Zuma apelekwe mahakamani kujibu mashtaka hayo.
``Kama rais hana hatia kama anavyodai, basi aiache mahakama ithibitishi usafi wake,`` amesema Mmusi Maimane, Kiongozi wa DA.
Awali, Wakili wa serikali, aliyaweka pembeni madai hayo yaliyotolewa Aprili 2009 na kumpa Zuma nafasi ya kuendelea kuwania urais wa nchi hiyo. Zuma alikuwa akikabiliwa na madai zaidi ya 780 ya rushwa.
Rais Zuma na Mamlaka ya Mashtaka ya Taifa, (NPA) walikata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu uliochukuliwa Aprili 2016.
Hata hivyo jaji Lorimer Leach alikataa uamuzi huo na kusema si sahihi kwa NPA kuziweka pembeni tuhuma hizo.
Nafasi ya NPA katika kesi ya Zuma
NPA ina wajibu wa kuamua iwapo itaendelea na mashtaka hayo yanayohusiana na ubadhirifu wa karibu dola 2 bilioni za ununuzi tata wa silaha uliogharimu mlipa kodi mabilioni ya dola kutoka shirika moja la Ufaransa.
Hata hivyo haikufahamika mara moja iwapo Zuma atakwenda katika Mahakama ya Katiba kujaribu tena kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu.
NPA inatakiwa kutilia maanani uamuzi wa msemaji wa Serikali, Luvuyo Mfaku aliyehimiza muda wote kuheshimiwa kwa sheria na kuzingatia maslahi ya utawala wa sheria.
Jaji Leach alisema: `` Ni vigumu kuelewa kwa nini utawala wa sasa wa NPA umechukulia kuwa uamuzi wa kutengua mashtaka hayo unaweza kutetewa,``
Kashfa hizo za rushwa dhidi ya Zuma tangu aingie madarakani zimejikita zaidi katika barua pepe zilizovuja zikihusisha pia familia ya Gupta, biashara za marafiki wa rais huyo ambao wanadaiwa walitumia nafasi hiyo kupata mikataba minono katika kampuni zao.
Mwandishi: Florence Majani(Rte/Ap)
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.