ANC yataka ZANU PF kujadiliana na upinzani Zimbabwe
10 Julai 2008Viongozi wa chama tawala nchini Afrika Kusini cha African National Congress ANC wamekihimiza chama cha rais Mugabe cha ZANU PF kufanya majadiliano na upande wa upinzani.
Hatua inachukuliwa na wengi kama ishara kuwa chama cha ANC kinaweza kikatoa mchango mkubwa katika mgogoro wa kisiasa nchini Zimbabwe.
Taarifa za viongozi wa chama cha ANC kuhimiza wenzao wa ZANU PF kufanya majadiliano na upande wa upinzani zimetolewa mjini Harare ,mji mkuu wa Zimbabwe.
Kwa mujibu wa gazeti la serikali la ya Zimbabwe la Herald toleo la leo alhamisi naibu mkuu wa chama cha ANC Kgalema Motlanthe,ametoa mwito huo baada ya yeye na katibu mkuu wa ANC Gwede Mantashe kukutana na rias Mugabe jumatano mjini Harare.
Gazeti limeendelea kumnukuu afisa huyo akisema kuwa chama chake cha ANC nacho kinaunga mkono misimamo ya SADC na Umoja wa Afrika kuwa njia pekee ya kutanzua mgogoro wa Zimbabwe ni mdahalo kati ya ZANU PF na vyama vya upinzani.
Akijibu suali la ikiwa mazungumzo ndio suluhisho la mgogoro wa ushindi wa Mugabe wa tarehe 27 Juni ambao mataifa ya magharibi uchaguzi huo hayautambui,Motlanthe amenukuliwa kusema kuwa Umoja wa watu wao ndio kitu muhimu na ndio nguzo ya maendeleo.
Kiongozi wa uopinzani Morgen Tsvangirai alikataa kumtambua Mugabe kama mshindi wa duru ya pili ya uchaguziambayo alijiondoa dakika za mwisho kutokana na vitisho.Aidha amekataa kufanya mazungumzo na serikali ikiwa matokeo ya juzi yataheshimiwa.
Rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki amekuwa mpatanishi wa mgogoro huo kwa kipindi cha zaidi ya mwaka sasa lakini ameshindwa kupata ufumbuzi. Na kuhusika kwake kumekosolewa na MDC kikisema kuwa anampendelea Mugabe.
Na hayo yakiarifiwa kuna taarifa kuwa mazunguzo kati ya ZANU PF na MDC yameanza alhamisi nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa duru zilizoko karibu na majadiliano hayo zimeliarifu shirika la habari la AFP kuwa wajumbe wa pande zote mbili walisafiri jumatano kwenda Afrika Kusini kutokea Zimbabwe.
Duru za chama cha MDC zinasema mtu wao Tendai Biti aliondoka Harare kwenda Afrika kusini mapema alhamisi kwa kile zilichokiieleza kama mazungumzo ya awali kabla ya majadialano mengine muhimu.
Biti ambae anakabiliwa na kesi ya uhaini aliondoka Harare baada ya mahakama ya Zimbabwe kukubali kumrejeshea hati yake ya kusafiria.
Nao viongozi wa mataifa ya G8 waliokutana nchini Japan wiki hii walitaka mjumbe maalum kusiadia katika juhudi za upatanishi,huku pia wakipinga uhalali wa serikali ya Mugabe na hivyo kutishia vikwazo zaidi dhidi ya utawala wake.
Na mabalozi wamesema kuwa huenda leo baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likapiga kura kuhusu vikwazo ambavyo vinamlenga Mugabe pamoja na watu wake 13.