Ancelotti akasirishwa na kipigo dhidi ya Liverpool katika FA
6 Januari 2020Mwishoni mwa juma hili ilirindima michezo ya kombe la FA ambapo Crystal Palace imejiunga na orodha ya vikosi vya Premier League vilivyoyaaga mashindano hayo msimu huu baada ya kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Derby County katika duru ya tatu hapo jana. Chelsea iliishinda Nottingham Forest kwa mabao 2-0 na Sheffield United iliionesha mlango wa kutokea Fylde na kufikia duru ya nne, lakini Tottenham Hot Spur itabidi kurejea mchezo wake dhidi ya Middlesbrough baada ya kutoka sare ya bao 1-1.
Aston Villa na Brighton zilisalim amri baada ya kuondolewa katika kinyang'anyiro hicho. Leo Arsenal inapimana nguvu na Leeds United, wakati Tottenham itabidi warejee uwanjani kesho Jumanne kuamua nani ni nani dhidi ya Middlesbrough. Manchester United nayo itarejea uwanjani kesho kuoneshana kazi na Wolverhampton baada ya kumaliza mchezo wao kwa sare ya bila kufungana.
Kocha wa Everton Carlo Ancelotti anapanga uchunguzi wa haraka kuhusiana na kikosi chake kilivyopata kipigo cha kufadhaisha katika kombe la FA dhidi ya makinda wa Liverpool. Kikosi cha Ancelotti kilipoteza nafasi adimu kushinda mchezo huo uwanjani Anfield kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999 wakati chipukizi mwenye umri wa miaka 18 Curtis Jones alipoifungia Liverpool bao la ushindi jana Jumapili katika mchezo wa watani wa jadi, Derby.
Klopp alifanya mabadiliko ya wachezaji 9, akianza na kikosi chenye thamani ya pauni milioni 43.9 , wakati Everton kikosi chake kina thamani ya pauni za Uingereza milioni 222. Everton haijashinda dhidi ya Liverpool tangu mwaka 2010, na kuifanya Derby ya Merseyside kuwa chungu kwa kocha huyo aliyetokea Napoli Carlo Ancelotti, ambaye yuko tayari kujadili jinsi wachezaji wake walivyocheza.
Nae mlinzi wa Manchester United Harry Maquire anaweza kukosa pambano la nusu fainali ya kombe la ligi mchezo wa mkondo wa kwanza dhidi ya Manchester City baada ya kuumia katika mchezo wa kombe la FA mwishoni mwa juma, amesema kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer.