1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Andrea Nahles ajiuzulu Nyadhifa zote katika Chama cha SPD

Oumilkheir Hamidou
2 Juni 2019

Mwenyekiti wa chama cha Social Democrat-SPD ambae pia ndie mkuu wa kundi la wabunge wa chama hicho, Andrea Nahles ameamua kujiuzulu nyadhifa zote hizo mbili baada ya mivutano ya muda mrefu ya kuania madaraka chamani.

Berlin Andrea Nahles SPD-Vorsitzende
Picha: Reuters/F. Bensch

"Mijadala miongoni mwa wabunge na  taarifa zinazonifikia zinanidhihirishia kuna ukosefu wa imani kuweza kuendelea kutekeleza nyadhifa zangu ipasavyo"-ameandika Andrea Nahles katika risala aliyowatumia wanachama wa SPD.

Amewajulisha  Jumatatu atawasilisha risala ya kujiuzulu kama mwenyekiti wa chama mbele ya kamati ya uongozi na Jumanne atajiuzulu kama mwenyekiti wa kundi la wabunge. Kwa namna hiyo anasema anataka kurahisisha zoezi la kumchagua au kuwachagua watakaokamata nyadhifa  hizo lifanyike kwa njia inayostahiki.

Andrea Nahles anapanga pia kuachana na wadhifa wake kama mbunge wa SPD.

Habari za kuaminika zinaashiria uwezekano wa waziri mkuu wa jimbo la Rheinland Pfalz, Malu Dreyer kukabidhiwa kwa muda wadhifa wa mwenyekiti mkutano wa dharura wa chama cha SPD utakapoitishwa na wadhifa wa mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha SPD akabidhiwe naibu mwenyekiti wa kundi hilo Rolf Mützenich pindi hadi Jumanne inayokuja hakutokuwa na yeyote atakaejitokeza kuwania wadhifa huo.

Andrea NahlesPicha: Reuters/F. Bensch

Heko na sifa kwa Andrea Nahles

Katika wakati ambapo mtaalam wa masuala ya kiuchumi wa benki ya ING Carsten Brzeski anaulinganisha uamuzi wa kujizulu Andrea Nahles kama "zahma ziada katika medani ya kisiasa nchini Ujerumani", wanasiasa wa vyama mbali mbali wanamsifu mwanasiasa huyo kwa uamuzi wake.

Mwenyekiti wa chama cha kiliberali FDP, Christian Lindner anamtaja Andrea Nahles "kuwa mwanasiasa muaminifu na mwenye uwezo. Kujiuzulu kwake sio jibu la suala kuhusu mwongozo wa chama cha SPD, badala yake uamuzi huo unazidi kuidhoofisha serikali ya muungano."

Walinzi wa mazingira die Grüne pia wamemvulia kofia Andrea Nahles. Viongozi wenza wa chama hicho Annalena Baerbock na Robert Habeck wameelezea matumaini yao kuona suala la nani anakabidhiwa wadhifa gani katika chama hicho kikongwe zaidi cha kisiasa nchini Ujerumani linapatiwa ufumbuzi haraka.

"Heko, Andrea Nahles. Uamuzi wako unastahili sifa. Siasa isiachiwe kuwa katili. Pengine uamuzi wako utatufanya tutafakari."Ameandika mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha mrengo wa kushoto Die Linke Dietmar Bartsch.

Katika wakati ambapo chama cha CDU kinaelezea matumaini ya kuendelezwa serikali ya muungano, waziri wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje Michael Roth, wa chama cha SPD amemshukuru Andrea Nahles kwa bidii za kutaka kukikwamua chama hicho na kukosoa malumbano ya ndani dhidi yake.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa/

Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW