1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Andrea Nahles kuongoza SPD

22 Aprili 2018

SPD imemchagua mwanamke kwa mara ya kwanza katika historia yake ya miaka 155 kuwa mwenyekiti. Mivutano iliyopo ndani ya chama hicho ni mzigo mkubwa unaomsubiri kiongozi mpya

Andrea Nahles
Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Probst

Kwa mara ya kwanza katika historia ya miaka 155 ya chama cha Social Democratic SPD nchini Ujerumani kimemchagua mwanamke kukiongoza chama hicho. Katika mkutano maalum wa chama uliofanyika leo Jumapili(22.04.2018) katika mji wa Magharibi mwa Ujerumani wa Wiesbaden wanachama wa SPD wamepiga kura kuchagua kati ya wagombea wawili -Andrea Nahles ambaye ni kiongozi wa chama hicho bungeni au meya wa jiji la Flensburg Simone Lange.

Mshindi wa nafasi ya mwenyekiti wa SPD ana majukumu ya kutuliza mivutano ya ndani ya chama  wakati ambapo chama hicho kinapambana kujiweka katika nafasi nzuri baada ya kupata  kipigo na kuporomoka kufuatia matokeo mabaya ya uchaguzi mkuu uliofanyika mnamo mwezi Septemba mwaka 2017 sambamba na kujengeka upinzani wa wanachama wanaopinga chama hicho kuingia katika serikali ya mseto na wahafidhina wanaoongozwa na kansela Angela Merkel.

Mivutano

Mwanzoni mwa mkutano tawi la vijana la wanachama wa SPD wanaopinga hasa chama hicho kuwa sehemu ya serikali mpya Ujerumani waliwataka wajumbe kumpinga Andrea Nahles. Nahles anaungwa mkono na uongozi wa juu wa SPD  wakati meya Lange mwanachama wa SPD ambaye hana umaarufu anaungwa mkono na wana-SPD sio zaidi ya 100 kati ya wajumbe 7,700.

Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Takriban wajumbe 600 wa SPD na wanachama 45 wa bodi kuu ya utendaji ya chama hicho wanahaki ya kupiga kura katika mchakato wa leo.Nahles mwenye umri wa miaka 47 amechaguliwa kwa asilimia 66.

Amechaguliwa  kwa matumaini makubwa ya kufufua imani ya wapiga kura kuelekea chama hicho. Ikumbukwe kwamba katika uchaguzi mkuu  uliopita SPD kilipata asilimia 20.5 pekee ya kura,hayo yakiwa ni matokeo mabaya kabisa kuwahi kuonekana katika chama hicho tangu kuungana kwa Ujerumani mbili. Uungwaji mkono wa SPD ulipwaya zaidi wakati kulipozuka mivutano ya ndani kuhusu uundaji serikali ya mseto na Kansela Merkel na matokeo yake chama hicho kilifikia kuporomoka na kupitwa wakati mmoja hata na chama kinachopinga wahamiaji cha AFD(chama mbadala kwa Ujerumani)

Uchunguzi wa maoni nchini Ujerumani uliochapishwa Alhamisi 19.04.2018 umeonesha kwamba wapiga kura asilimia 47 wanamashaka ikiwa kweli Nahles anaweza kukiunganisha chama hicho na kukiondowa katika mivutano. Wakati huohuo uchunguzi wa maoni pia unaonesha ni asilimia 17 ya wajerumani wanaimani na chama cha SPD wakati asilimia 32 wanaunga mkono kundi la Kansela Merkel la vyama ndugu vya kihafidhina CDU/CSU.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Isaac Gamba

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW