Andry Rajoelina achaguliwa tena kuwa rais wa Madagascar
25 Novemba 2023Rajoelina ameshinda kwa asilimia 58.95 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais wa Novemba 16, kulingana na matokeo yaliyowasilishwa na tume ya uchaguzi, na ambayo yanahitaji kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo. Waliojitokeza kupiga kura walikuwa zaidi ya asilimia 46, ikiwa ni idadi ya chini ikilinganishwa na uchaguzi uliopita wa mwaka 2018, ambao tume ya uchaguzi ililaumu mazingira mabaya ya kisiasa na udanganyifu.
Rajoelina mwenye umri wa miaka 49 amesema: "Watu wa Madagascar wamechagua njia ya mwendelezo na utulivu", baada ya matokeo kutangazwa. Rajoelina aliingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2009 kufuatia mageuzi yaliyomuondoa madarakani rais wa zamani Marc Ravalomanana. Kisha akaruka chaguzi zifuatazo ili tu kurejea mshindi katika uchaguzi wa 2018.
Wapiga kura milioni 11 walipaswa kuchagua kati ya Rajoelina na wagombea wengine 12. Wapinzani kumi kati ya 12 walikataa kufanya kampeni na kuwataka wapiga kura kutoshiriki uchaguzi huo, wakiuita kuwa ni mchezo wa kuigiza.
Andry Rajoelina, meya wa zamani wa mji mkuu Antananarivo, anatuhumiwa na wapinzani kwa ufisadi na kufumbia macho uporaji wa maliasili za nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na misitu yake ya thamani ya ''rosewood.''
Upinzani walalamikia mapinduzi ya kitaasisi
Wapinzani wamehoji na kutangaza kwamba hawatambui matokeo ya uchaguzi huo waliouita kuwa haramu, uliojaa karoso na kutupilia mbali machafuko yoyote ya kisiasa na kijamii yanayoweza kutokea.
Upinzani bado haujaonyesha kama utapinga matokeo rasmi na haujaitisha maandamano zaidi mitaani. Wiki chache kabla ya upigaji kura, upinzani -- ikiwa ni pamoja na marais wawili wa zamani - waliongoza karibu kila siku, maandamano makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa yalipigwa marufuku na kutawanywa na polisi.
Madagascar imekuwa katika msukosuko tangu ripoti za vyombo vya habari mwezi Juni kufichua kuwa Rajoelina alipata uraia wa Ufaransa mwaka 2014. Wapinzani wamedai kuwa, chini ya sheria za nchi hiyo, rais alipaswa kupoteza uraia wake wa Madagascar, na pamoja na hayo, uwezo wa kuongoza nchi.
Wagombea wa upinzani walilalamikia "mapinduzi ya kitaasisi" yaliyompendelea rais aliyeko madarakani, wakiishutumu serikali kwa kufanya kazi ya ''kumteua tena Rajoelina''. Walitaka mchatakato wa uchaguzi usitishwe na jumuiya ya kimataifa kuingilia kati.
''Uchaguzi ulifanyika katika hali ya uwazi''
Nchi nane na mashirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya na Marekani walielezea wasiwasi wao kuhusu ''matumizi yasiyo ya uwiano ya nguvu'' ya kutawanya maandamano ya upinzani. Upinzani umelaani ukiukwaji wa sheria, ikiwa ni pamoja na kufungwa kwa vituo vya kupigia kura, ukosefu wa masanduku ya kura na matumizi ya rasilimali za serikali na Rajoelina kwa kampeni yake.
Mmoja wa wapinzani wawili waliosalia rasmi kwenye kinyang'anyiro hicho, Siteny Randrianasoloniaiko, pia alishutumu "machafuko yanayotia wasiwasi" ambayo amesema "yanazua maswali halali kuhusu uhalali wa matokeo". Arsene Dama, mwenyekiti wa tume ya kitaifa ya uchaguzi, amesema siku ya Jumamosi kuwa uchaguzi ulifanyika "katika hali ya kawaida na ya uwazi". Hata hivyo suala la kutoegemea upande wowote kwa Dama limetiliwa shaka na upinzani.
Chanzo : AFPE