Merkel kukutana na Gordon Brown.
13 Machi 2009Kansela Angela Merkel wa Ujerumani leo anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Uingereza, Gordon Brown, mjini London , katika jumla ya hatua za kutayarisha mkutano wa nchi za G 20 utakaofanyika mwezi ujao .
Wakati huo huo, mawaziri wa fedha wa nchi hizo ishirini pia wanakutana katika mji huo. Tofauti zimejitokeza kabla ya kufanyika mkutano huo wa mwezi Aprili juu ya mkakati wa kukabiliana na mgogoro wa uchumi ulioikumba dunia.
Kansela Merkel amepinga pendekezo la Marekani juu ya kutoa fedha zaidi kwa ajili ya kuukabili mgogoro wa uchumi , badala yake nchi yake pamoja na Ufaransa zinataka taratibu za kudhibiti mabenki ziimarishwe zaidi.
Bibi Merkel amesema Ujerumani itaukabili mgogoro huo mnamo mwaka 2009 na 2010 katika msingi wa mipango yake miwili iliyokwishapitisha.
Mkutano wa nchi 20 tajiri na zinazoinukia kiuchumi mwezi Aprili utakuwa mtihani mkubwa kwa dunia inayokabiliwa na mgogoro mkubwa wa uchumi usiokuwa na mithili tokea kumalizika vita kuu ya pili.
Abdu Mtullya/Silke Engel /ZA.