Angela Merkel akutana na Mohammed Mursi
30 Januari 2013Wanajeshi walikuwa wamejipanga nje ya ofisi ya Kansela Merkel mjini Berlin, kumpokea rais Mohammed Mursi. Merkel na mgeni wake walitembea katika zulia jekundu huku tarumbeta zikiburudisha. Hii ni mara yake ya kwanza kwa Mursi kuitembelea Ujerumani. Baada ya kula chakula cha mchana pamoja, Merkel na Mursi walizungumza na waandishi wa habari.
Awali Mursi alikuwa amepanga kubakia Berlin kwa muda wa siku mbili lakini hali tete ya usalama nchini mwake imemlazimisha kurejea nyumbani leo. Alikuwa amedhamiria pia kuitembelea Ufaransa siku ya Ijumaa, lakini safari hiyo imebidi ifutwe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kansela Merkel alisema kwamba anataka kuona mazungumzo yakifanyika na vyama vyote vya kisiasa. Pamoja na hayo ameitaka serikali ya Mursi iheshimu haki za binadamu. Masuala ya kiuchumi yalizungumziwa pia. "Kwa mtazamo wangu, ukuaji wa kiuchumi ni jambo linalowawezesha wananchi kuwa na maisha mazuri. Ni muhimu mgogoro wa uchumi uepukwe. Kwa njia hiyo uchumi utasaidia pia kuimarisha hali ya kisiasa."
Mbali na mgogoro wa kisiasa unaoendelea, tatizo kubwa linaloikabili Misri kwa sasa ni la kiuchumi. Idadi ya watalii imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya mapinduzi kutokea mwaka 2011. Hivi sasa Misri inahitaji wawekezaji kutoka nje. Hapa Ujerumani, wafanyabiashara wanaelewa kwamba Misri ni mahala pazuri pa kuwekeza lakini wanahofia hali ya usalama.
Mursi aahidi demokrasia zaidi
Nchini Misri kwenyewe viongozi wa vyama vya upinzani wametangaza kuwa tayari kufanya mazungumzo na serikali. Mohammed El Baradei ambaye ni kiongozi katika chama cha ukombozi wa kitaifa ametoa tangazo hilo siku mbili tu baada ya upinzani kusema kwamba hauko tayari kwa mazungumzo.
Katika mkutano wake na Kansela Merkel, rais Mursi ameahidi kuharakisha juhudi za kuleta demokrasia nchini mwake, akisema kuwa Misri inataka kuwa nchi inayofutata utawala wa sheria. "Misri itakuwa nchi inayoruhusu uhuru wa kutoa maoni," alieleza Mursi akiishukuru Ujerumani kwa kuwa mshirika wake katika juhudi za kuleta demokrasia.
Kiongozi huyo ametaja pia kwamba yuko tayari kupanua mahusiano baina ya nchi yake na Ujerumani lakini akasisitiza kwamba ushirikiano huo hautakiwi kuwa kigezo cha nchi moja kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine. Mursi anakutana pia na wawakilishi wa sekta mbali mbali za kiuchumi hapa Ujerumani kutafuta wawekezaji.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa
Mhariri: Saumu Yusuf