Angela Merkel ana umaarufu kuliko Rais Trump
2 Oktoba 2018Utafiti huo unaonesha kuwa taswira ya Marekani imeshuka zaidi miongoni mwa washirika wake baada ya mwaka ambapo Rais Trump alizidisha mashambulio yake ya maneno kwa mataifa kama vile Canada na Ujerumani. Walipoulizwa mtizamo wao kuhusu viongozi watano duniani, asilimi 52 ya waliohojiwa walisema kwamba wana imani na Merkel katika utekelezaji wake, huku asilimia 27 pekee wakieleza imani yao kwa Trump.
Rais Trump aliorodheshwa wa mwisho miongoni mwa viongozi hao watano . Orodha hiyo iliwajumuisha Rais wa Urusi Vladimir Putin ambapo asilimia 30 walisema wana Imani na uongozi wake , Rais wa China Xi Jinping aliyepata asilimia 34 na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Trump alikuwa na viwango vidogo nchini Mexico ambapo asilimia sita pekee ya watu walisema wana Imani na uongozi wake, wakati Israe vilevile ikiwa na ubaguzi wa nadra kumhusu kiongozi huyo wa Marekani. Baada ya mwaka mmoja tangu Trump alipoamua kuuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv hadi Jerusalem, hatua yake ya kuidhinisha hatua hiyo ilizidisha kukubalika kwake kwa asilimia 69 nchini Israel kutoka asilimia 56 mwaka uliopita.
Utafiti huo unaonesha Merkel alikuwa na umaarufu katika mataifa ya Uholanzi, ambapo asilimi 85 walimtizama vyema, lakini hakupendelewa kwa wingi nchini Ugiriki, ambapo ni asilimi 15 pekee waliohojiwa walisema wanamuamini. Tangu kuchukua hatamu za uongozi mwaka uliopita, Trump ameiondoa Marekani kwenye mikataba mbalimbali ya kimataifa,ukiwemo ule unaohusiana na tabia nchi wa Paris na mkatabawa nyuklia wa Iran.
Mwezi Juni baada ya mkutano wa G7 nchini Canada, Trump alikataa kutia saini taarifa ya pamoja na washirika wa Marekani, na kumtaja mwenyeji wake Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, kuwa asiye mkweli na dhaifu. Mara kwa mara amekuwa akiishambulia Ujerumani kwa biashara ya ziada,kutotumia fedha nyingi katika masuala ya ulinzi na kutegemea gesi kutoka Urusi.
Marekani yapendelewa kuwa na nguvu za kuongoza
Wiki iliyopita, alipokuwa akihutubia baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Trump alichekwa na viongozi wa kimataifa aliposema amefanikisha mengi katika miaka miwili aliyokuwa madarakani kuwahi kufanywa na yeyote katika historia ya waliowahi kuwa viongozi nhini Marekani.
Mataifa ambayo yametoa mtizamo mzuri kuhusu Marekani ni Israeli, Ufilipino na Korea Kusini ambapo wote wamempa asilimia 80. Licha ya Trump kuorodheshwa wa mwisho miongoni mwa viongozi hao watano, asilimia 63 ya watu waliohojiwa walisema dunia itakuwa na ubora iwapo Marekani itasalia kuwa na nguvu za kuongoza, ikilinganishwa na asilimia 19 ambao waliitaka China kuwa na jukumu hilo. Utafiti huo ulifanywa kati ya mwezi Mei na Agosti, na kuzingatia mahojiano ya zaidi ya watu mia tisa katika mataifa 26.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/RTRE/DPAE
Mhariri: Mohammed Abdulrahman