1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angela Merkel atimiza miaka 10 kama Mwenyekiti wa CDU

11 Aprili 2010
Mwenyekiti wa chama cha CDU na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.Picha: AP
Dr Helmut Kohl ,Desemba 2009.Picha: AP

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametimiza miaka 10 tangu ashike uongozi wa chama cha Christian Democratic Union-CDU, huku mafanikio yake yakienda sambamba na historia ya kuungana tena kwa Ujerumani. Katika kipindi hicho cha miaka 10 cha bibi Merkel kama Mwenyekiti wa chama, amejitokeza katika hali mpya ya kujiamini mbele ya jukwaa la kimataifa.

Wakati Bibi Merkel , mwanafizikia kutoka Ujerumani mashariki ya zamani, alipojiunga na CDU baada ya kuanguka ukuta wa Berlin 1989, chama hicho cha kihafidhina, kilikuwa kikidhibitiwa na Helmut Kohl, mkongwe wa siasa za Ujerumani na muasisi wa Muungano wa Ujerumani.

Chini ya uongozi wa Kohl, Merkel akawa waziri wa masuala ya wanawake mwaka wa 1991 na 1994 akaiongoza wizara ya mazingira. Katika mwaka 1994 akateuliwa katibu mkuu wa chama cha CDU.Ni wakati huo ambapo Bibi Merkel aliweza kuonyesha ujasiri wake katika siasa. Wakati alipojiunga na baraza la mawaziri kwa mara ya kwanza alijieleza kuwa ni mtu "mwenye moyo mzito wa kuyakabili mambo."

Mwaka 1999 Merkel aliyeitwa jina la utani "Binti wa Kohl" akajitenga na mwalimu wake huyo hadharani, ilipobaini kwamba Kohl alipokea zaidi ya DeutschMark milioni 2, fedha zilizotolewa na watu fulani kukifadhili chama, bila ya kujulikana majina yao. Kashfa hiyo ingeweza kukiathiri vibaya mno chama cha CDU na badala yake ikasababisha Bibi Merkel kuchukua Uongozi wa chama akiwa Mwenyekiti Aprili 10, 2000.

Ingawa mwanafunzi huyo wa Kansela wa zamani Helmut Kohl, alifuata njia yake ya kutatua migogoro lakini Merkel hakufuata nadharia kamili ya mwalimu wake ambaye alishuhudia vita vya pili vya dunia na akajitolea kuhakikisha Ujerumani inaijongelea zaidi Ulaya.

Merkel alichukua madaraka ya Ukansela kuiongoza Ujerumani 2005 na wakati wa kipindi chake cha kwanza madarakani akaitumia vizuri ile fursa ya Ujerumani kuandaa fainali za kombe la kandanda la dunia 2006 na urais wa kundi la nchi nane zilizoendelea kiviwanda G8 ambao huzunguka miongoni mwa wanachama, kujijenga kimataifa na kudhihirisha uwezo wake kisiasa.

Ikiwa ni miezi sita sasa tangu kuanza kipindi chake cha pili cha Ukansela, ameendelea kudhihirisha umahiri wake hasa baada ya kuzuka msukosuko wa kiuchumi duniani na kuwasilisha mpango wa Ujerumani kama mfano bora kwa Ulaya. Alibakia mkakamavu wakati wa msukosuko wa kiuchumi ulipoikumba Ugiriki na kusisitiza juu ya haja ya Ulaya kuhakikisha sarafu ya euro inabakia imara.

Mchango wa jeshi la Ujerumani, Bundeswehr kimataifa pia umebadilika chini ya uongozi wake na hivi sasa limejiingiza pia katika mapambano nchini Afghanistan chini ya uongozi wa jumuiya ya kujihami ya magharibi, NATO.

Ushirika wake hivi sasa na chama cha Free Democrats -FDP- kinachopendelea wafanyabiashara na ambacho kimerudi serikalini baada ya miaka 11 ya kuwa upande wa upinzani,umeandamwa na mabishano kuhusu suala la kodi, mageuzi ya mfumo wa afya na ustawi wa jamii.

Lakini Kansela ameonekana kusimama kidete katika msimamo wake na badala yake anayelaumiwa kwa sehemu kubwa ni Kiongozi wa FDP, Waziri wa mambo ya nchi za nje Guido Westerwelle.

Uchaguzi wa mkoa wa Northrhine Westphalia mwezi ujao , utatoa jibu kama mkakati huu wa muda mrefu ni wa manufaa kwa Bibi Merkel, kabla ya uchaguzi mwengine mkuu wa Ujerumani 2013.

Wakati huo atakuwa anatafuta ridhaa ya wapiga kura kwa kipindi cha tatu,lakini hadi wakati huo, bado Bibi Merkel yuko mbali na mtangulizi wake Kohl, aliyekuwa Kansela wa Ujerumani kwa miaka 16 na kiongozi wa chama cha CDU kwa robo karne -miaka 25. Merkel ametimiza miaka 10 ya uongozi wa CDU na ndiyo kwanza miaka 4 na miezi 6 ya Ukansela.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman /Reuters

Mpitiaji : Peter Moss

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW