Angela Merkel ziarani Tokyo
31 Agosti 2007
Kanzela Angela Merkel wa Ujerumani, ameanzisha juhudi mpya kuona hatua madhubuti zinachukuliwa ulimwenguni kupambana na uchafuzi wa hali ya hewa.Akizuru wakati huu Japan, baada ya ziara yake ya China, Bibi Merkel,alipendekeza jana kuwa upunguzaji wa moshi unaochafua hewa uambatane na idadi ya wakaazi wa kila nchi.Hivyo, ni kusema kila nchi ilenge kupunguza moshi unaochafua mazingira kwa muujibu wa wingi wa wakaazi wake.
Kanzela Angela Merkel,akaonya hii leo huko Tokyo, kwamba pale mapatano ya Kyoto yatakapomalizika 2012,nchi changa zitaziuliza nchi zilizoendelea kiviwanda zilizotia saini mapatano hayo iwapo zimetekeleza shabaha za mkataba huo za kupunguza moshi unaochafua mazingira.
Baadhi ya nchi zitapata taabu kujibu swali hilo na miongoni mwa nchi hizoni zile zanachama wa Umoja wa ulaya kama vile Spain ,Ureno na Ugiriki.
Kanzela Merkel na viongozi wengine duniani, zinapigania kuwa nchi changa nazo zinatoa mchango wao katika kufikia shabaha zinazolengwa kuwamo katika mkataba mpya.
Kwa muujibu wa mkataba wa Kyoto,nchi changa kama vile China na India-zote 2 zikiwa zimeuidhinisha mkataba huo,hazikutakiwa kupunguza moshi unaochafua hewa na kuchangia kutia ujoto duniani.
Kanzela Angela Merkel,amesema ulimwengu ujiandae barabara kwa majadiliano magumu.Akaongeza ,
“Tutazamie nchi changa zinazoinukia, hazitatwikwa moja kwa moja jukumu sawa na dola za kiviwanda.Lakini, jambo moja pia ni wazi kabisa:Sidhani,ikiwa tufikie mapatano ya haki,nchi kama hizo zinazonyanyukia kiuchumi, zitaweza kupunguza moshi wa viwandani kwa kima sawa na kile cha dola za kiviwanda zilizokwisha endelea kiviwanda.”
Kanzela Merkel akaongeza kuonya kwamba kwavile mengi yanategemea kupunguza uchafuzi huo,mazungumzo hayatakua rahisi lakini hakuna pia njia ya kuepuka.Alitaka wezani uwepo katika mkataba huo mpya ambamo kila nc hi itatoa mchango wake.
Nchi changa kwa jumla, hazitoi moshi mwingi ukilinganisha na nchi za kiviwanda.China tu kati ya kundi la nchi hizo ndio inayochafua zaidi mazingira.
Kwa kadiri Fulani,China hata imeipindukia Marekani mwaka huu.Lakini China ikiwa na wakaazi bilioni 1 na laki 3,kupunguza moshi wake kwa kipimo cha kila mkaazi wake,bado kutakua kasoro ya kipimo cha nchi za magharibi.
Ikiwa kituo chake cha mwisho cha ziara hii iliomchukua pia China,Kanzela wa Ujerumani, atazuru mji wa Osaka na kuhudhuria mashindano ya ubingwa wa riadha ulimwenguni ambamo wasichana wa Ujerumani hadi jana, walikwisha shinda medali 2 za dhahabu.