1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola, DRC kukarabati reli inayounganisha maeneo ya madini

14 Julai 2023

Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zinaweka matumaini ya kuendeleza uchumi wa nchi hizo mbili kutokana na mpango wa kukarabati reli inayounganisha maeneo muhimu ya madini na bahari ya Atlantic.

Tansania Eisenbahnbau
Picha: Xinhua/picture alliance

Mapema mwezi huu, Angola na Kongo zilifikia mapatano na wawekezaji, mapatano hayo ni ya mkataba wa miaka 30 wa kuendesha njia ya reli inayounganisha bandari ya Angola ya Lobito na mji wa Kolwezi, uliopo kwenye ukanda wa shaba nchini Kongo.

Mradi huo wa dola milioni 555, unaofadhiliwa kwa kiasi na Marekani unatarajiwa kuongeza mauzo ya nje ya madini na biashara ya ndani ya Afrika na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia baina ya Angola na nchi za Magharibi.

Soma pia:Tanzania na Burundi zasaini makubaliano ya ujenzi wa reli 

Mtaalamu wa jopo la Chatham la nchini Uingereza, Alex Vines amesema mradi huo unaoifungua bandari ya Lobito kwa  wawekezaji wa Marekani ni hatua mpya ya kihistoria.

Njia hiyo ya reli ya kiliometa 1700 ilikamilishwa karibu karne moja iliyopita na wawekezaji wa Uingeraza ili kusafirisha  shaba kutoka barani Afrika. Hata hivyo, sehemu ya Angola ya  njia hiyo ya reli ilifungwa kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe vya nchini Angola vilivyoanza mnamo mwaka 1975 hadi 2002.

Wasafiri wakiwa wamejazana kwenye treni nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.Picha: Desirey Minkoh/AFP/Getty Images

Baada ya kujengwa upya na kampuni moja ya China njia hiyo ya reli ilifunguliwa tena mnamo mwaka 2005 lakini imekuwa inakabiliwa na changamoto. Kwa sasa takriban ni treni moja tu inayopita kwenye reli hiyo kila baada ya wiki mbili.

Soma pia: Magufuli azindua reli ya kiwango cha kimataifa

Mkuu wa miundombinu wa kampuni ya taifa ya Kongo, Marcel Lungange amesema upande wa Kongo wa reli hiyo ulianza kutumika wakati wa ukoloni lakini matunzo hayakuwa mazuri. Amesema kwa wastani reli inaharibika mara tatu kwa siku.

Lunganga ameeleza kuwa treni zinajikokota kwa mwendo wa kilometa mbili kwa saa!

Kutokana na hali hiyo makampuni ya uchimbaji madini yanapendelea kusafirisha bidhaa kwa malori hadi kwenye bandari nyingine ambazo aghalabu hukabiliwa na misongamano katika nchi za Tanzania, Msumbiji na Afrika Kusini. Safari hizo ni ghali na zinachukua muda mrefu.

Mahitaji ya dunia yaongezeka maradufu

Mwenyekiti wa chama cha wafanya biashara nchini Kongo Louis Watum amesema njia za usafirishaji wa ufanisi zinahitajika kutokana na mahitaji ya madini muhimu kuongezeka.

Ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) nchini Tanzania

02:57

This browser does not support the video element.

Shirika la nishati la kimataifa linaratajia ongezeko la mara nne hadi kufikia mwaka 2040 wakati ambapo dunia inafanya juhudi za kukabiliana na mabadliko ya tabia nchi. 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ndio mzalishaji mkuu wa madini ya cobalti na shaba barani Afrika. Madini hayo yanatumiwa kwa ajili ya kutengeza mabapa ya nishati ya jua, milingoti ya nishati ya upepo na magari ya umeme. Mwenyekiti wa chama cha wafanyabishara wa Kongo Watum amesema, tayari pana msongamano mkubwa wa malori mipakani.

Mradi wa reli unaopewa pumzi mpya utaimarisha huduma kati ya Angola na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Lengo ni kuwezesha treni sita kwa siku katika reli hiyo inayoziunganisha Kongo na Angola kwa kutumia muda usiozidi saa 36.

Soma pia: Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakubaliana ujenzi wa miundombinu

Na kwa ajili hiyo kiasi cha dola milioni 445 kitatolewa na wawekezaji. Nusu ya kima hicho kitachangiwa na kampuni ya mandeleleo ya Marekani.

Mradi wa ukarabati wa reli kati ya Angola na DRC unalenga kuimarisha ufikiaji wa maeneo muhimu yanayozalisha rasilimali za madini ili kukidhi mahitaji ya ulimwengu.Picha: HOUSSEM ZOUARI/AFP

Chini ya mpango huo ukarabati wa reli nchini Angola utafanyika pamoja na kununua mabehewa na injini za treni zaidi ya 1500. Fedha zingine zitatengwa kwa ajili ya mradi wa kuiunganisha Zambia.

Mradi huo unadhihirisha dhamira ya rais wa Marekani Joe Biden ya kuitekeleza ahadi ya nchi yake ya kuhusika kikamilifu  katika kuimarisha biashara baina ya Marekani na bara la Afrika.

Mradi huo pia unaonesha mabadiliko katika mlengo wa kidiplomasia wa Angola. Kutokana na reli hiyo Angola na Kongo pia zitaimarisha uhusiano wao wa kiuchumi.

Chanzo: AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW