Angola yawasilisha mapendekezo ya kuumaliza mzozo wa Kongo
6 Januari 2026
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Rais wa Angola, Tshisekedi alikutana na mwenyeji wake Joao Lourenco katika mji mkuu wa Angola, Luanda na kwamba mkutano kati ya viongozi hao wawili ulidumu kwa saa kadhaa.
Hata hivyo haijafahamika mara moja ni mapendekezo gani yaliyowasilishwa kwa Tshisekedi.
Mkutano kati ya Tshisekedi na Lourenco — ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Umoja wa Afrika — umefanyika siku chache kabla ya mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa eneo la Maziwa Makuu unaotarajiwa kufanyika Alhamisi, kwa lengo la kujadili hatua za kukabiliana na hali ya usalama inayozidi kuzorota mashariki mwa Kongo.
Juhudi za awali za Angola za kupatanisha pande zinazohasimiana hazijawahi kuzaa matunda, licha ya mazungumzo kadhaa kufanyika katika miaka ya karibuni.
Eneo la mashariki mwa Kongo lenye utajiri mkubwa wa rasilimali ambalo linapakana na Rwanda na Burundi, limekumbwa na machafuko kwa miongo kadhaa.