1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Anis Amri hakuonekana kitisho kwa maafisa

Sekione Kitojo
29 Desemba 2016

Wataalamu wa kupambana na ugaidi nchini Ujerumani wanaamini kwamba mtuhumiwa wa shambulizi la mjini Berlin Anis Amri  hakuonekana kuwa ni kitisho na kuwa na uwezo wa kufanya mashambulizi.

Deustchland | Anschlag mit LKW auf Weihnachtsmarkt in Berlin
Gari lililogonga watu katika soko la krismass mjini BerlinPicha: picture-alliance/rtn-radio tele nord rtn/P. Wuest

 Inadaiwa  kwamba  dakika  chache   kabla  Amri hajaligonga  gari  lake  aliloteka  nyara  katika  soko  la Krismass   mjini  Berlin, alituma  ujumbe  wa  sms , akisema : " Ndugu  zangu, kila  kitu  kiko  sawa , kwa mujibu  wa  mapenzi  ya  Mwenyezi  Mungu. Hivi  sasa niko  katika  gari , niombeeni ndugu  zangu, niombeeni."

Ujumbe  huo , pamoja  na  picha  ya  kujipiga  aliyoipiga akiwa  ndani  ya  lori  hilo, huenda  ilitumwa  kwa  Mtunisia mwenye  umri  wa  miaka  40  aliyekamatwa  mjini  Berlin jana  Jumatano, limeandika  gazeti  la  Sueddeutsche Zeitung.

Waombolezaji wakiwa wameweka mishumaa kuomboleza vifo vya watu waliokuwa katika soko la Krismass mjini BerlinPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Wachunguzi wanaotafuta  kugundua  iwapo  Amri  alikuwa na  mshirika  wamesema  mtuhumiwa  aliyekamatwa  raia wa  Tunisia "anaweza  kuwa  alihusika  katika  shambulio hilo". Lakini maafisa  wa Ujerumani  wamemwachia  huru mtu  huyo  mwenye umri  wa  miaka  40 raia  wa  Tunisia leo, siku moja  baada ya  kukamatwa.

Maafisa  wa  kupambana  na  ugaidi  wana  taarifa  za  kina kuhusu Amri,  walifahamu  kuwa  anahusiana  kwa  karibu na  mtandao  wa  Waislamu  wenye  itikadi  kali  nchini Ujerumani  na   aliwahi  kuwa  anatafuta  maelekezo  katika mtandao  juu  ya  jinsi  ya  kutengeneza  mabomu  ya mabomba, gazeti  hilo  limeripoti.

Maelezo  ya  hivi  karibuni  kabisa  ya  Amri, ambayo  ni pamoja  na  taarifa  kuhusiana  na  utambulisho  wake unaotofautiana  mara  nane, ulifanyiwa  mapitio Desemba 14, siku  tano  tu  kabla  ya  kuuwa  watu  12  katika shambulio  la  mjini  Berlin.

Waendesha  mashitaka  magharibi  mwa  Ujerumani wamesema  wamefungua  uchunguzi  wa  udangayifu mapema  mwaka  huu  dhidi  ya  Anis Amri , mtuhumiwa mkuu  katika  shambulio  la  wiki  iliyopita  mjini  Berlin.

Mhusika katika shambulizi la soko la KrismassPicha: picture alliance /Bundeskriminalamt

Waziri  Mkuu  wa  Italia,  Paolo Gentiloni  amesema  leo kwamba  mtuhumiwa  wa  shambulizi dhidi  ya  soko  la Krismasi  mjini  Berlin  hakuwa  anasaidiwa  na  mtandao wa  washirika  nchini  Italia.

Gentiloni  aliwaeleza  waandishi  habari  mjini  Rome kwamba  hadi  hivi  sasa  hakuna  ushahidi  kwamba  kijana huyo  mwenye  umri  wa  miaka  24 raia  wa  Tunisia alikuwa  na  mahusiano  na  mtandao  wowote  nchini  Italia ambao  ulikuwa  ukimsaidia.

Wakati  huo  huo  polisi  mjini  Kolon imepiga  marufuku maandamano  ya  kundi  la  siasa  kali  za  mrengo  wa kulia  katika  mkesha  wa  mwaka  mpya  wakati  wakijaribu kuzuwia  kurejewa  kwa  ghasia  za  mwaka  jana  na kusema  wataweka  vizuwizi  kuzuwia  mtu  yeyote  kuweza kuendesha  gari  kwa  lengo  la  kuwashambulia  watu.

Vizuwizi vimewekwa kuzuwia mashambulizi mengine dhidi ya masoko ya KrismassPicha: DW/N. Jolkver

Maafisa  wa  jiji  tayari  wamekwishatangaza  mipango  ya kuweka  polisi  1,500 mara  10  zaidi  kuliko  ilivyokuwa mwaka  jana  wakati  polisi  waliposhindwa  kuzuwia uporaji na  mashambulizi  ya  kingono  ambayo  wanalalamikiwa watu  wenye  asili  ya  kigeni.

Mwandishi:  Sekione Kitojo /  Ape / Afpe / Rtre

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo