1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Anjouani yavamiwa

25 Machi 2008

Kisiwa cha Comoro cha Anjouan kimevamiwa na majeshi ya Umoja wa Afrika na ya Comoro kumaliza uasi wa M.Bacar

Taarifa za hivi punde kutoka Moroni, mji mkuu wa visiwa vya Comoro, viliopo kiasi cha maili 500 kusini-mashariki mwa Dar-es-salaam,zinasema kikosi cha askari 400 cha Umoja wa nchi za kiafrika kikijumuisha wanajeshi wa Tanzania,Sudan na jeshi la Comoro kimeingia Anjouan mapema alfajiri ya leo na tayari kimeuteka mji mkuu Mutsamadu , miji 2 mengine -Domoni na Ouani na hata uwanja wa ndege ili kuzima uasi wa Kanali Mohammed Bacar. Wakaazi wa kisiwa Anjouan waliingia kwa wingi mitaani kuyakaribisha majeshi hayo ya Umoja wa Afrika.

►◄

Vikosi vya Umoja wa Afrika pamoja na vile vya jeshi la Comoro, viliwasili kwa marekebu kisiwani Anjouan alfajiri ya leo na taarifa za hivi punde zasema, vimeshakidhibiti kisiwa kizima cha Anjouan.Kwa msaada wa askari 1,350 wa Umoja wa Afrika-wengi kutoka Tanzania na Sudan,serikali kuu ya Comoro mjini Moroni, inatumai haraka kumaliza kabisa uasi wa Mohamed Bacar,askari wa kuzuwia fujo-gendarm-aliefunzwa na wafaransa na alien'gangania madaraka ya kisiwa hicho kupitia uchaguzi usio halali wa mwaka jana na kuongoza kikosi cha waasi cha wanamgambo kiasi cha 700.

Mawasiliano ya simu na Anjouan yamekatwa na haikuweza kujulikana hatima ya Mohamed Bacar au ile ya washirika wake wa chanda na pete,Uwanja wa ndege wa Ouani unadhibitiwa na vikosi vya Umoja wa afrika na Comoro sawa na mji mkuu Mutsamadu.

Msemaji wa serikali ya Comoro, Bacar Dossar amesema baadhi ya wanajeshi wamepewa amri ya kumsaka kiongozi huyo muasi pale alipo.Ikifahamika kwamba mnamo miezi iliopita hakuwa akilala nyumbani mwake kwa hofu.

Kabla majeshi hayo ya Tanzania,Sudan na ya Comoro kuingia Anjouan alfajiri ya leo ili kukikomboa kisiwa hicho-mojawapo ya visiwa 3 vya Comoro au Ngazija,rais Ahmed Abdallah Sambi,binafsi kutoka kisiwa cha Nzouani,jana alitoa amri kwa vikosi vinavyosaidiwa na UA kuanza mashambulio huko Anjouan.Alipeleka huko ndege ya helikopta ikitawanya vipeperushi kuwaonya wakaazi kubakia majumbani mwao.

Rais Sambi alisema na ninamnukulu,

"Mnamo masaa au siku zijaszo ,kisiwa cha Anjouan kitakombolewa kwa matumizi ya nguvu au natumai waasi watajisalimisha ili kuepusha mpambano."

Serikali kuu ya Comoro, mjini Moroni, inamtuhumu Mohammed Bacar kuwa na azma ya kujitenga na visiwa vya comoro.Binafsi lakini, anadai azma yake sio kujitenga bali kudai mamlaka zaidi ya kujiendeshea kisiwa hicho mambo yake ya ndani.

Vikiwa nje ya pwani ya Afrika mashariki,visiwa vya Comoro-Ngazija,Moheli na Anjouani (Nzouani), asili yake vilikuwa visiwa 4 pamoja na Mayotte ambacho kimesalia kwenye mamlaka ya Ufaransa,baada ya visiwa vyengine 3 kujitangazia uhuru kutoka Ufaransa, 1975.

kiuchumi , visiwa vya Comoro vinalima mazao ya vanilla,karafuu na ylang-ylang.

Visiwa vya comoro vilikaliwa mwanzo na wasafiri kutoka Arabuni kiasi cha miaka 1,000 iliopita naabadae, viligeuka pepo ya maharamia.vikiwa na jumla ya wakaazi laki 7, ni mwanachama wa umoja wa Afrika (AU)na Jumuiya ya nchi za kiarabu-Arab League.

Baada ya kujionea njama kiasi 20 za mapinduzi ya kijashi mengine ya askari wa kukodiwa tangu uhuru 1975,serikali kuu ya Comoro ya rais Mohammed Sambi inajaribu sasa kurejesha utulivu masiwani na kuseleleza umoja wa visiwa vya Comoro.