Ankara. Iran na umoja wa Ulaya wakaribia kuwa na mawazo ya pamoja.
27 Aprili 2007Mjumbe wa majadiliano ya kinuklia wa Iran Ali Larijani amesema kuwa Iran na umoja wa Ulaya wanakaribia kuwa na mawazo ya pamoja katika maeneo fulani ya mazungumzo yao na mawazo mapya yametolewa ili kuvunja hali ya mkwamo wa kimataifa kuhusiana na mpango wa kinuklia wa Iran.
Mratibu wa masuala ya sera za kigeni wa umoja wa Ulaya Javier Solana amesema kuwa mazungumzo hayo yamekuwa mazuri na yamefanyika katika mazingira mazuri, licha ya kuwa hakuna maendeleo makubwa yaliyofikiwa kwa sasa.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema kuwa imefahamishwa kuhusu mazungumzo hayo na haina habari juu ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa. Mazungumzo hayo yatafanyika tena katika muda wa wiki mbili zijazo. Maafisa waandamizi wa mataifa matano wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la umoja wa mataifa pamoja na Ujerumani wanatarajiwa kukutana mjini London wiki ijayo kuangalia upya mazungumzo ya Solana na Larijani.