ANKARA : Iran yataka fikra kwa mzozo wake wa nuklea
26 Aprili 2007Msuluhishi mkuu wa masuala ya nuklea wa Iran amesema anataraji jumuiya ya kimataifa kuwasilisha fikra mpya zenye lengo la kutatua mzozo wa kidiplomasia juu ya mpango wa nuklea wa Iran.
Ali Larijani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Uturuki Ankara ambapo anakutana na mratibu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Havier Solana kwa mazungumzo ya siku mbili ya kutafuta utatuzi wa mzozo huo. Solana amesema anatumai watapiga hatua za maendeleo kuweka msingi wa mazungumzo kamili hapo baadae.
Hata hivyo wachunguzi wa mambo wanasema pande hizo mbili bado zinatafautiana sana.Mataifa mengi ya magharibi yanahofu kwamba Iran yumkini ikawa inataka kutengeneza silaha za nuklea.
Serikali ya Iran inasisitiza kwamba mpango wake huo wa nuklea ni kwa ajili ya dhamira za amani tu.