ANKARA : Uturuki kujaribu utatuzi wa kidiplomasia
22 Oktoba 2007Uturuki itatumia njia zote za kidiplomasia kutatuwa mzozo wa waasi wa Kikurdi walioko kaskazini wa Iraq kabla ya kuanzisha operesheni za kijeshi.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Ali Babacana amekaririwa na vituo vya televisheni vya CNN na vile vya Uturuki wakati wa ziara yake nchini Kuwait akisema kwamba watajaribu njia zote za kidiplomasia kabla ya kufanya operesheni yoyote ile ya kijeshi.
Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye yuko kwenye shinikizo la umma kuamuru shambulio la kijeshi ndani ya mpaka wa Iraq dhidi ya makambi ya waasi wa Kikurdi wa chama cha PKK yalioko nchini humo leo ameitisha mkutano wa dharura kabla ya kundoka kuelekea Uingereza kwa ziara rasmi.
Waturuki leo kwa siku ya pili wamemiminika mitaani ambapo takriban Waturuki 3,000 kwenye mji wa Instanbul wamekuwa wakitowa kauli mbiu dhidi ya PKK na kumkosowa Erdogan kwa kutochukuwa hatua ya kijeshi mara moja.
Habari kutoka Washington zinasema Marekani itashirikiana na Uturuki na Iraq katika kukabiliana na waasi hao wa Kikurdi kufuatia mapambano ya mpakani ambapo Uturuki inasema wanajeshi wake 12 wameuwawa na wanane hawajulikani walipo.